Tanga. Takribani theluthi moja ya madaraja wilayani Handeni Vijijini, Mkoa wa Tanga, yako katika hali mbaya inayohatarisha maisha ya wananchi, hususani wakati wa msimu wa mvua, Mwananchi limebaini.
Uchunguzi wa Mwananchi uliofanyika kwa miezi mitatu umebaini kuwa mvua, ambazo kwa wakulima ni baraka, zimegeuka kuwa chanzo cha hofu, kukatika kwa mawasiliano na kusimama kwa shughuli za kijamii na kiuchumi katika baadhi ya vijiji.
Chanzo kikuu cha hali hiyo ni ubovu wa miundombinu ya madaraja, mengi yakiwa yamechakaa au kujengwa kwa mfumo wa muda mfupi, hivyo kutokuwa salama.
Baadhi ya maeneo hakuna madaraja, bali vivuko vilivyojengwa kwa kutumia miti, mbao na magogo, hali inayoongeza hatari wakati wa mvua.
Takwimu za Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), Wilaya ya Handeni, zinaonesha asilimia 70 ya madaraja wilayani humo yamefanyiwa marekebisho, huku asilimia 30 yakiwa mabovu.
Meneja wa Tarura, Wilaya ya Handeni, Mhandisi Judica Makyao, anakiri uwepo wa changamoto hiyo akieleza:
“Asilimia 70 ya madaraja wilayani hapa tumeyafanyia marekebisho. Yaliyobaki, likiwemo daraja la Mto Mligazi, yapo katika hatua ya tathmini. Kutokana na changamoto za kifedha, tunalazimika kuangalia maeneo yenye uhitaji wa dharura zaidi,” anasema.
Hatari huongezeka kipindi cha mvua ambacho wananchi hulazimika kutumia madaraja yasiyo rasmi kuvuka mito.
Vijiji vya Kwasunga, Miono na Kwamsisi ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na kukosekana kwa daraja katika Mto Mligazi linalounganisha wilaya za Handeni na Bagamoyo.
Kwa wakazi wa vijijini, daraja si miundombinu pekee bali ni uti wa mgongo wa maisha yao ya kila siku. Ni njia ya wanafunzi kufika shuleni, wagonjwa kupata huduma za afya, wakulima kusafirisha mazao na wafanyabiashara kufikia masoko ya nje ya vijiji vyao.
Kwa zaidi ya miongo sita tangu Tanzania Bara (Tanganyika) ipate Uhuru mwaka 1961, eneo hilo halijawahi kujengwa daraja la kudumu, badala yake wananchi wamekuwa wakitengeneza vivuko vya muda kwa kutumia miti, mbao, magogo na udongo.
Kutokana na malighafi inayotumika katika ujenzi huo, baada ya muda mfupi huoza na kubomoka, hususani msimu wa mvua.
Mwananchi limeshuhudia hali hatarishi ya daraja hilo ambalo mbao na magogo yameshaoza, baadhi ya miti imekatika na nguzo zimeanza kuelemea upande mmoja, hali inayoongeza hatari kwa pikipiki na bajaji zinapopita.
Kauye Semboga, mkazi wa Kijiji cha Kwamsisi, anasema kukosekana kwa daraja katika Mto Mligazi ni kikwazo kwa elimu ya watoto wao.
“Nasomesha kijana aliye kidato cha sita. Nimelazimika kumpeleka kwa shangazi yake Miono kwa sababu wakati wa mvua hawezi kwenda shule. Kivuko tulichotengeneza kikibomoka hakuna njia ya karibu zaidi, zaidi ya kuzunguka Mkata ambako ni mbali,” anasema.
Kwa upande wake, Hadija Salum, mkazi wa Kwekonje, Kata ya Kwasunga, anasema wananchi wamechoka kuishi katika hofu ya kupoteza maisha.
“Unavuka huku unaomba Mungu. Mtoto au pikipiki ikiteleza unaanguka mtoni. Kipindi cha mvua mawasiliano yanakatika kabisa. Tumechoka kuishi kwa hofu,” anasema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Juma Mohamed, anadai daraja hilo limekuwa nyenzo ya kisiasa wakati wa kampeni bila kuchukuliwa hatua za utekelezaji.
“Viongozi wanakuja kuchukua kura, lakini baada ya uchaguzi hakuna kinachofanyika. Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie, tatizo hili limekuwa sugu,” anasema.
Kwa kauli hizo za wananchi, daraja la Mto Mligazi si tu kero ya miundombinu, bali ni tishio kwa maisha, elimu na uchumi wa eneo hilo.
Kwa kutokuwapo daraja, shughuli za kiuchumi zimeathirika, wakulima wakilazimika kuuza mazao yao kwa bei ya chini kutokana na gharama kubwa za usafiri.
“Hata kama mazao yakiwa mengi, wafanyabiashara hawatakuja kwa sababu ya barabara na daraja. Tunauza kwa hasara, baadhi ya wakulima wameacha kulima mihogo kwa sababu hailipi. Gari moja likijaa unamuuzia kwa Sh70,000 badala ya Sh100,000,” anasema Malua Said.
Vilevile, ukosefu wa miundombinu bora umechangia vifo vya wajawazito na wagonjwa wanaoshindwa kufikishwa kwa wakati katika vituo vya afya vilivyo mbali.
“Nimemzika mwanangu hivi karibuni kwa sababu ya ukosefu wa daraja. Nakumbuka ilikuwa wakati wa mvua mwaka 2022, binti yangu alikuwa mjamzito, alitokwa damu nyingi hadi akapoteza fahamu. Ikabidi apelekwe Mkata, sasa hadi ambulansi inafika zahanati alikuwa tayari amepoteza damu nyingi,” anasema Pili Mungeni, mkazi wa Kitongoji cha Kimbuguru, Kata ya Kwasunga.
Pili Mrisho, mkazi wa Pozo, anadai kila mwaka watu watatu au zaidi hupoteza maisha kwa kukosekana daraja, akiwanyooshea kidole cha lawama viongozi kwa madai ya kutowajibika ipasavyo.
“Kuna mbunge aliyepita, hata bungeni hatujawahi kumsikia akizungumzia changamoto ya daraja hadi tunajiuliza shida nini? Watu wanakufa eneo hili, lakini ni kama hawajali,” anasema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwasunga, Ntumbo Mnenga, anakiri kuwa tatizo la daraja ni la muda mrefu, akieleza kuwa jitihada za wananchi na viongozi wa kijiji bado hazijazaa matunda kutokana na ukosefu wa fedha.
“Changamoto ni ya muda mrefu na taarifa za daraja hili zipo ngazi za juu. Viongozi wanafahamu, tumekuwa tukishirikiana nao pamoja na wananchi. Tutaendelea kufuatilia hadi hatua za utekelezaji zichukuliwe,” anasema na kuongeza:
“Tumempa taarifa mbunge wa sasa, amesema kalibeba na atakwenda kulifanyia kazi na kulisemea bungeni ili, panapo majaliwa, liwe kwenye hatua za utekelezaji.”
Hussein Kamnama, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwasampa, kilichopo Kata ya Kwasunga, anasema bado viongozi hawajapata fedha kutoka halmashauri kwa ajili ya ujenzi zaidi ya kuchangishana wenyewe.
“Baada ya uchaguzi wa Serikali za mtaa (2024) tumefikisha mwaka, lakini hili daraja ni kero kubwa. Kijijini limekuwa gumzo. Baadhi ya watu wamefanya jitihada kujenga daraja la miti wakati tunasubiri fedha za ujenzi kutoka Serikali Kuu, angalau tuweke la muda tukiendelea kusubiri daraja la kudumu,” anasema.
Anaeleza: “Hatujapata fedha kutoka juu zaidi ya kuchangishana kwenye halmashauri za vijiji vitatu vya Kwandugwa, Kwanyanje na Kwasunga. Kila kimoja tulichangisha Sh1 milioni kwa ajili ya ujenzi.”
Meneja wa Tarura, Wilaya ya Handeni, Mhandisi Makyao, anasema hatua za awali za kitaalamu zimefanyika, akibainisha kuwa daraja hilo lipo katika eneo zuri kwa ujenzi.
“Ni kweli daraja la Mto Mligazi linalounganisha wilaya za Bagamoyo na Handeni ni kikwazo kikubwa kwa wananchi, lakini ulishafanyika utafiti wa kijiolojia kubaini uimara wa miamba na matabaka ya chini ili kuhakikisha daraja litakalojengwa litakuwa salama,” anasema.
“Baada ya kufanya uchunguzi wa awali, tukagundua daraja lina urefu wa zaidi ya mita 50 na haliwezi kusanifiwa katika ngazi ya wilaya, hivyo usanifu wake unafanyika Tarura makao makuu. Tuliwatumia maombi mwaka 2022, nafikiri ni suala la sisi kufuatilia maendeleo yake,” anasema.
Makyao anaeleza kuna mradi wa uboreshaji wa barabara vijijini kwa ushirikishaji wa jamii na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi (Rise), ambao upo hatua za mwisho za usanifu, na ukikamilika utajumuisha daraja hilo.
“Kama utakamilika mapema na kwa wakati, basi matumaini yetu ni kwamba changamoto ya daraja hilo na barabara yake kwa ujumla itakuwa imetatuliwa,” anasema.
Makyao anasema awamu ya kwanza ya barabara za Sindeni–Kwedikwazu (kilomita 38) na Michungwani–Kwadoya (kilomita 19) zipo hatua za mwisho za usanifu wa awali, akieleza kuwa awamu ya pili itajumuisha daraja la Mligazi na barabara yake.
Anasema barabara za Mkata–Kwasunga (kilomita 21), Kabuku–Mzungi (kilomita 18) na Kwachaga–Kwamkonje (kilomita 10.1) zabuni ilitangazwa, lakini mkandarasi bado hajapatikana.
Vilevile, anaeleza Tarura haina bajeti ya kutosha, hivyo inasubiri fedha kutoka Serikali.
“Tarura huwa tunaangalia mahitaji muhimu zaidi. Mfano, kuna madaraja ya Mto Mchafu, Mto Mbabwi na Gole, hayo ni madaraja tunayoyapa kipaumbele zaidi kwa sababu yamekuwa yakisababisha ajali na watu wanakufa,” anasema.