Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekata mzizi wa fitina, baada ya kumteua Dk Lazaro Komba aliyeshika nafasi ya tano katika kura za maoni kuwania ubunge wa Peramiho, Mkoa wa Ruvuma huku aliyeongoza kwa kura, Victor Mhagama akiachwa.
Uamuzi huo wa Kamati Kuu ya CCM, unamuondoa Victor katika mbio za kurithi nafasi iliyoachwa wazi na mama yake, Jenista Mhagama aliyefariki dunia Desemba 11, 2025 akiwa mbunge wa Peramiho kwa miaka 20.
Katika mchakato wahuo wa ndani wa CCM, Victor aliongoza kwa kupata kura za maoni 3,040, huku aliyeteuliwa Dk Komba ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, alishika nafasi ya tano kwa kura 213.
Hata hivyo, mchakato wa kura za maoni katika jimbo hilo, uliibua tuhuma za rushwa, vijembe, kuchafuana na lugha zisizofaa kutoka kwa baadhi ya wanachama na kuzua hofu ya kuzaliwa mpasuko ndani ya chama hicho tawala.
Tuhuma hizo, ziliifanya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuingilia kati na kuwahoji baadhi ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya na watia nia wenyewe akiwemo Victor.
Mbio za ubunge katika jimbo hilo, ziliwakutanisha makada 27 wa CCM, ukiacha Victor na Dk Komba, wengine ni Getrude Haule aliyeoata kura 2,913, Dk Joseph Mhagama (943), Frank Matola (215), Dk Damas Mapunda (200) na Isabellah Mwampamba (131).
Wengine ni Joseph Masikitiko (126), Erasmo Mwingira (124), Allen Mhagama (114), Schoral Ngonyani (84), Lazaro Ndenji(68), Davis Ngonyani(62), Thea Ntara (57), Emil Ngaponda (51), Serafina Mkuwa (48), Clemence Mwinuka (35), Emelian Mbawala (24), Benjamin Kamtawa(23), Prosper Luambano(22), Dominic Mahundi( 19),Fredrick Millinga (17),Sixmund Rungu (9),Rose Shawa (7), Rosemary Ngonyani(6), Enoc Moyo (6).
Taarifa ya uteuzi wa mgombea huyo, imetolewa leo Jumapili Januari 25, 2026 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi baada ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika visiwani Zanzibar na kuongoza na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la Julai 2025, Kamati Kuu imefanya uteuzi Dk Lazaro Komba kuwa mgombea wa CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Peramiho, lililopo Wilaya ya Songea Vijijini,” amesema.
Sambamba na hilo, kikao hicho kimeteuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), wanaotokana na Bunge nafasi tatu kutoka Tanzania Bara.
Walioteuliwa kwa wanaume ni mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda na mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, huku Asia Halamga akiteuliwa kuwa MNEC kwa upande wa wanawake.
Kwa upande wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa wanaotokana na Bunge kutoka Zanzibar, wameteuliwa Khamis Mussa Omar na mwanamke ni Tauhida Cassian Galos na Agnes Hokororo ameteuliwa kuwa Katibu wa wabunge wote wa CCM.
Kwa upande wa Wenyeviti wa Bunge wameteuliwa, Najma Giga, Deodatus Mwanyika na Cecilia Pareso
Kamati Kuu hiyo pia imewateuwa wajumbe wa NEC wanatokana na Baraza la Wawakilishi, ambao ni Said Ali Juma na Hamza Hassan Juma, huku mwanamke ni Lela Muhamed Mussa.
Kwa upande wa Wawakilishi wa CCM watakaoingia bungeni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bakar Hamad Bakar, Dk Shaame Ali Ali, Simai Mohammed Said na Fatma Ramadhan Mandora.
Katibu wa wawakilishi wote wa CCM, aliyeteuliwa ni Machano Othman Said na wenyeviti wa Baraza la Wawakilishi ni Mahmoud Omar Hamad na Hudhaima Mbarak Tahir.