Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ameiasa jamii kuachana na dhana potofu ya kuficha wagonjwa wa ukoma na kujitokeza wanapobaini viashiria vya ugonjwa huo ili kurahisisha jitihada za Serikali kutokomeza ugonjwa huo nchini.
Waziri Mchengerwa amesema hayo leo Jumapili, Januari 25, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati akitoa tamko la maadhimisho ya siku ya ukoma duniani.
Waziri Mchengerwa amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kaya zote zilizo katika maeneo wanakoibuliwa wagonjwa wapya wa ukoma zinafuatiliwa na wanakaya wote kufanyiwa uchunguzi na kubaini wenye kuugua ugonjwa huo na kuwaanzishia matibabu.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati akitoa tamko la maadhimisho ya siku ya ukoma duniani.
“Tukifanya hivyo kila mkoa na halmashauri na kila mahali tunaweza kutokomeza ugonjwa huu hata kabla ya mwaka 2030,” amesema Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amesema wagonjwa wote wanaoibuliwa wanatambuliwa makazi, kijiji, na kata anakotoka, ndani ya wilaya husika au nje ya mkoa, ambapo iwapo mgonjwa atatokea nje ya mkoa, ihakikishwe ya kuwa taarifa zake zinapelekwa alikotokea ili kufanya ufuatiliaji na kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa huo kuwapatia tibakinga kaya husika.
Aidha, Mchengerwa amesema tangu mwaka 2006, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitangaza Tanzania kuwa tayari imefikia kiwango cha kimataifa cha kutokomeza ugonjwa wa ukoma cha chini ya mgonjwa mmoja kati ya watu 10,000.
Pia idadi ya wagonjwa wapya wanaogunduliwa nchini inaendelea kupungua kutoka wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,442 mwaka 2025 sawa na punguzo la asilimia 37.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wakati akitoa tamko la maadhimisho ya siku ya ukoma duniani.
Waziri Mchengerwa amewashukuru watoa huduma katika vituo vya huduma za afya nchini kwa juhudi za kuboresha afya za wananchi na kuhakikisha ugonjwa wa ukoma unapungua kasi ya kusambaa nchini.
Huku akiwapongeza wanahabari kwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu afya bora na namna ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa ukoma.
“Mikoa na halmashauri inabidi mhakikishe kila mgonjwa anayeibuliwa anatambulika anakotoka na taarifa zake zifanyiwe kazi ili kukata mnyororo wa maambukizi, niwashukuru watoa huduma kwa juhudi zenu za kutibia wananchi na wanahabari ambao mnasambaza elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huu,” amesema Mchengerwa.