MAHUBIRI: Mshirikishe Mungu kujitoa maagano yanayoleta uharibifu

Bwana Yesu Kristo asifiwe karibu popote ulipo katika tafakari ya neno la Mungu. Tunapouanza mwaka ni muhimu uwe na masomo ya msingi ambayo yatakusaidia katika kipindi cha mwaka mzima ili uweze kuyatimiza malengo ambayo umejiwekea.

Somo la leo linaeleza namna unavyotakiwa kumshirikisha Mungu ili kujitoa kwenye maagano ya giza uliyoingia kwa kujua au kutokujua kisha kukuletea uharibifu na kuharibu ushirika wako na Mungu.

 Agano ni mfumo unaonganisha mtu zaidi ya mmoja au mtu na mfumo kwa kuzingatia kanuni zilizopo kwa kuhakikisha kuwa mtazamo, msimamo na njia ni moja.

 Kumbukumbu la Torati 12:2-3

Nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.

Nyakati hizi kumekuwa na wimbi kubwa la ndoa kuvunjika kwa sababu mbalimbali lakini unapokutana na watumishi wa Mungu yapo mengi yanayoendelea yasiyoonekana yanayotokana na watu kufarakana watakufunulia yakiwamo hayo maagano ya uharibifu.

Mwanzo 6:4-7…Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa.

Namna mtu anavyoweza kuingia agano lenye uharibifu

Kukiri mwenyewe, kukiriwa na mtu mwingine, kukirishwa kawaida au kwenye ndoto. Damu ya kafara, damu ya hedhi, damu ya mtu mwenyewe. Kula kwenye Matambiko, Ndotoni. Kutoa Sadaka kwenye madhabahu ya kiganga, manabii wa uongo, familia kujiunganishwa kwenye mizimu na miungu kwa sadaka zao.

 Dalili kuwa kuna agano lenye uharibifu

Kufanya mambo usioyapenda ila unajikuta unafanya. Kupita kwenye njia usiyotaka moyoni mwako. Kushindwa kuokoka kikamilifu, unataka ujae Roho wa Mungu wa mbinguni lakini unashindwa.

Kutopenda kutumia au kutaja jina na Damu ya Yesu Kristo wakati unaomba…unaishia kusema Baba, Bwana badala ya katika Jina la Yesu Kristo

Kuota ndoto mbaya kama kula, uko shimoni, umezungukwa na watu, unashindwa kuvuka kwenda upande wa pili.

Kupoteza nguvu za kuomba na kutumia akili zaidi kuliko imani. Kutopenda Ibada yaani Neno, maombi na kutoa sadaka.

Ni damu ya Yesu Kristo pekee ndiyo inayoweza kuvunja hayo maagano kati ya nafsi na mwanadamu na viumbe  wabaya katika ulimwengu wa roho.

Waebrania 7:22,25 basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.

Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai siku zote ili awaombee.

Kwa maana hiyo sasa ili mtu apate msaada lazima akubali kutengeneza agano na Mungu wa mbinguni kupitia damu ya Yesu Kristo.

Hivyo ili uwe huru ni  lazima uvunje agano lenye uhalibifu halafu uingie katika agano jingine naMungu kwani hakuna mwanadamu asiyekuwa na agano yaweza kuwa ya nuru au giza.

 Njia za kuweka agano na Mungu

Kuamini katika roho na kweli kuwa damu ya Yesu Kristo ipo hai na inaokoa. Kukiri kwa kinywa chako kuwa Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Warumi 10:10… Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kutokea hapo, unakuwa umeshatengeneza Agano na Mungu wa mbinguni linaloitwa Wokovu na mchakato wa kuwa huru inaanza yaani ufundishwe na kuombewa kwa maombi yenye nguvu na mamlaka.

Tunaona mifano dhahiri kama ilivyowatokea wana wa Israeli

Waamuzi 2; Yeremia 11
Waliacha agano la Mungu na kuabudu sanamu. Matokeo yake
walitawaliwa na maadui.Umaskini, vita na mateso.
Walichukuliwa utumwani.

Pia tunaona habari ya Sulemani kuachwa kwa Mungu  1 Wafalme 11.

Sulemani alianza vizuri lakini baadaye alifuata miungu ya wake zake. Alijenga madhabahu ya sanamu.Mungu alimkasirikia. Ufalme wake uligawanyika baada ya kifo chake. Amani ya maisha yake ilipotea.

Matokeo ya kuacha agano na Mungu

Tunaona katika jamii pindi inapotokea watu kumuacha huyu Mungu wa kweli na kufuata maagano ya giza matokeo yake ni kupata laana, kupoteza baraka, uharibifu wa familia na kifo cha kiroho au kimwili.

Tunapotafakari somo hili Mungu akupe neema ya kung’amua kila mahali ambapo uliingia maagano kwa kujua au kutokujua uanze safari ya kujitoa sasa kwa kufanya agano la kweli na Mungu ikiwa tunaelekea mwishoni mwishoni wa Januari, kwani bado hujachelewa. Weka agano na Mungu ili uweze kufanikiwa katika mambo yako.

Mungu wa mbinguni akubariki na kukufanikisha unapoielekea juma la mwisho katika mwezi huu wa kwanza katika mwaka wa 2026.