Miroshi aitaka Europa League | Mwanaspoti

KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga Goztepe inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki, Novatus Miroshi amesema lengo kubwa la timu hiyo ni kuhakikisha inafuzu michuano ya Ulaya msimu ujao.

Akizungumza baada ya mechi ya ligi kutamatika wakiondoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Rizespor, Miroshi amesema timu inapaswa kucheza kwa kiwango cha juu katika kila mechi ili kufanikisha ndoto ya kucheza michuano mikubwa Ulaya.

“Lengo letu ni kucheza Ulaya, tunapaswa kucheza kwa kiwango cha juu katika kila mechi, naishukuru timu kwa pamoja na juhudi kubwa tunazoonyesha,” amesema Miroshi.

“Tunapaswa kusonga mbele kwa umakini uleule katika kila mechi, kwani kila pointi ni muhimu kwetu na tunaamini tunaweza kufanya hivyo.”

Göztepe ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, nafasi ambayo kama itaendelea kuonyesha kiwango bora hadi mwisho wa msimu, itaiwezesha  kushiriki UEFA Europa League msimu ujao.

Kama timu hiyo itafuzu kucheza michuano hiyo hii itakuwa mara ya pili kwa Mtanzania huyo baada ya awali kucheza akiwa na Shakhtar Donetsk ya Ukraine msimu wa 2022/23 alipokuwa kwa mkopo akitokea Zulte Waregem ya Ubelgiji.

Nyota huyo alicheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto, chama hilo lilipotandikwa mabao 3-1 mechi aliyomaliza dakika zote 90.