Mradi kilimo biashara kunufaisha vijana 1,400

Morogoro. Vijana zaidi ya 1,400 wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kuwawezesha vijana katika uzalishaji wa mazao ya bustani kwa njia ya kilimo biashara.

Mradi huo unasimamiwa na Ushirika wa Wajasiriamali Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sugeco).

Mradi huo unatekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa hekari 200 lililopo Kijiji cha Lubungo, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kijana Shambani yaliyofanyika katika mashamba ya Sugeco  Januari 25, 2026, Mkurugenzi wa ushirika huo, Levocatus Kimario amesema changamoto kubwa inayowakabili vijana si umiliki wa ardhi, bali ni namna ya kuitumia ardhi hiyo kwa tija na kwa mtazamo wa kilimo biashara.

Kimario amesema lengo la mradi huo ni kuwawezesha vijana kwa kuwapatia ardhi pamoja na miundombinu ya msingi ya uzalishaji.

“Tunamkabidhi kijana eneo la kuanzia hekari moja hadi tatu ambalo tayari limeandaliwa kwa uzalishaji, na kumpa haki ya kulitumia kwa kipindi cha miaka mitatu,” amesema Kimario.

Pichani ni baadhi ya Vijana kutoka Kijiji cha Lubungo wakiwa pamoja na viongozi wa SUGECO kwenye moja ya Bwawa la kuhifadhia maji linalotumika katika kilimo cha mazao ya kibiashara. Picha na Jackson John.



Amesema ndani ya kipindi hicho, kijana anatarajiwa kuzalisha, kupata kipato na kuweka msingi imara wa kiuchumi utakaomuwezesha kununua na kumiliki ardhi yake mwenyewe, huku eneo la mradi likibaki kuwa daraja la kuwawezesha vijana wengine baada ya muda wake kukamilika.

Amesema mradi huo unalenga kutoa ajira kwa vijana 1,400 na unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh1.1 bilioni hadi kukamilika kwake.

Amesema Sugeco inashirikiana na Halmashauri husika kuwawezesha vijana kupata mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya kuendeleza mashamba wanayopewa.

Amesema kaulimbiu ya Sugeco ni kuhakikisha kilimo biashara kinaanzia sokoni, ambako kila zao linalolimwa na huandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko ili kumlinda mkulima dhidi ya hasara.

“Hapa kila zao linalolimwa lazima liwe na uhakika wa soko. Tunataka kijana awekeze akiwa anafahamu wazi anazalisha kwa ajili ya nani,” ameongeza.

Katika hatua ya awali, mradi umeanza na uzalishaji wa mazao ya bustani ya kibiashara ikiwemo nyanya na hoho, huku mipango ikiendelea ya kuanzisha uzalishaji wa mazao mengine kulingana na mahitaji ya soko, ikiwemo zao la pilipili mwendokasi ambalo tayari lina uhakika wa kuuzwa.

Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Lubungo na mnufaika wa mradi huo, Hadija Mohamed amesema mradi wa Sugeco umeleta mapinduzi makubwa katika kilimo cha vijana kijijini hapo.

Amesema awali walikuwa wakilima kwa kutegemea mvua, hali iliyowalazimu kulima msimu mmoja kwa mwaka, lakini kwa sasa wanalima mwaka mzima kwa kutumia umwagiliaji, hali iliyoongeza uzalishaji na kipato.

Pichani ni baadhi ya Vijana kutoka Kijiji cha Lubungo wakiwa pamoja na viongozi wa SUGECO kwenye moja ya Bwawa la kuhifadhia maji linalotumika katika kilimo cha mazao ya kibiashara. Picha na Jackson John.



Ameiomba halmashauri kuendelea kuwawezesha vijana ili waweze kuendeleza miradi yao na kujikwamua kiuchumi.

Naye Maulid Idrisa, mkazi wa kijiji hicho ameishukuru Sugeco kwa kuanzisha mradi huo, akisema umefungua fursa mpya za kiuchumi kwa vijana.

Amesema atawekeza nguvu zote katika shamba atakalopatiwa ili kutimiza malengo yake ya maisha kupitia kilimo biashara.