Nabi atia neno usajili wa Depu Yanga

KOCHA wa zamani wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Nabi amemmezea mate straika mpya wa kikosi hicho, Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ akisema Jangwani watafurahia ujio wa Muangola huyo ambaye anamfananisha na Fiston Mayele.

Depu ni miongoni mwa mastaa wapya waliotua Yanga dirisha dogo akitokea Radomiak Radom ya Poland aliyoichezea kwa miezi sita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi aliyekuwa Yanga kuanzia Aprili 20, 2021 hadi Juni 15, 2023, alisema Depu ni miongoni mwa wachezaji aliowataka Kaizer Chiefs ya Sauzi wakati anainoa, lakini ilishindikana.

meisema mshambuliaji huyo anaweza kuwa msaada mzuri kwa Yanga kwani Clement Mzize bado hajarudi uwanjani, hivyo wakisaidiana na Prince Dube basi watafanya kitu kikubwa hasa kwenye michuano ya CAF.

“Yanga imepata mshambuliaji mwenye makali kama ya Mayele ambaye ni Depu. Wakati nafika Kaizer Chiefs nilikuta wanatafuta mshambuliaji, maskauti wa timu hiyo walileta jina lake lakini klabu ikashindwa kumsajili kwa kuwa waliona gharama ni kubwa,” alisema Nabi.

“Niliumia sana kumkosa kwa kuwa ubora wake ndio aina ya mshambuliaji ninayemtaka, kwani Depu ni mchezaji mwenye nguvu na mbinu za kuwatoka mabeki lakini pia anajua kufunga.

“Labda apate changamoto nyingine, ila akiwa na utulivu na akili ya kuendelea kuwa bora anaweza kufanya makubwa ndani ya Yanga. Ukweli ni kwamba Yanga imepata mchezaji mzuri.”

Nabi na Mayele walifanya kazi pamoja ndani ya Yanga ambapo mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, alitua Agosti 2021 akitokea AS Vita na kuondoka Julai 2023 akitimkia Pyramids ya Misri alipo sasa huku akiweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.

Katika misimu miwili Depu amechezea timu nne akianzia Gil Vicente ya Ureno aliyoitumikia muda mfupi akiifungia mabao matatu. Baada ya hapo alitua Poland, ambapo aliichezea kwa miezi sita, huku akifanikiwa kuifungia bao moja pekee kabla ya kutua Yanga dirisha dogo.

Alipotua Yanga, alianza kwa kucheza dhidi ya Mashujaa ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara na kufunga bao la mwisho katika ushindi wa 6-0 huku akiingia uwanjani kipindi cha pili na kucheza kwa dakika 35.

Pia alitoa asisti. Juzi dhidi ya Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alicheza dakika zote 90, Yanga ikipoteza ugenini mabao 2-0.

Ikumbukwe kuwa, Depu ana kibarua, kwani katika nafasi anayoichezea hayuko pekee yake, anachuana na mastaa wawili waliopo hapo muda mrefu, Prince Dube na Clement Mzize. Dube ametia kambani mabao matatu katika mechi tano za ligi alizocheza msimu huu na  moja hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa, huku uliopita akifunga mabao 13 katika ligi wakati Mzize akitupia 14.