Habari Anti, kwa masikitiko makubwa ninakueleza kuwa nakosa uamuzi ni kwa namna gani nitamkwepa mama mkwe wangu anayenitaka kimapenzi.
Ulianza kama urafiki wa mama na mwanaye, tunatoka kwa ajili ya matembezi na kupata viburudisho, kumbe alikuwa na jambo lake sasa kanitamkia moja kwa moja kuwa ananitaka kibaya zaidi ananinyima amani maana amenikalia kooni.
Kwa mara ya kwanza maishani ninakosa jibu la moja kwa moja kumjibu mama mkwe wangu, naomba nisaidie nimjibu na nimalizane naye kwa amani, maana naona huko mbele ya safari hatutaelewana ukizingatia ndiyo anayetusapoti kwa kiasi kikubwa mimi na familia yangu akiwamo mke wangu (binti yake wa kumzaa).
Duniani kuna mambo, nami kwa mara ya kwanza nalazimika kutumia busara kukujibu, tofauti na hapo usingenisahau maishani mwako.
Maana sijui niseme umekosa nidhamu au haya kuruhusu kuwa karibu na mkweo kiasi hicho, amepeta nguvu ya kukueleza hayo kwa sababu hukuweka mipaka.
Unafanyaje urafiki na mama mkwe wako? Haya yanayotokea uliyataka.
Unatakiwa ujiulize kwa kina wewe ni nani, unaishi kwa misingi ipi na unataka heshima yako isimame wapi katika familia na jamii.
Kuruhusu urafiki wa karibu kati yako na mkwe wako si ustaarabu wala ujanja wa maisha, bali ni mlango wa matatizo makubwa yanayoharibu utu, ndoa na mustakabali wako.
Mkwe ni mzazi, ni mtu wa mipaka maalumu, si rafiki wa vicheko, matembezi, starehe au mazungumzo ya faragha.
Urafiki wa aina hiyo huvunja heshima taratibu, huondoa woga wa maadili na hatimaye huzaa tamaa, dharau na migogoro mikubwa ambayo huwezi kuimudu baadaye.
Mwanamume mwenye akili anatakiwa ajue kuweka mipaka mapema. Pale unapompa mkwe nafasi ya kuwa rafiki wa karibu, unajishusha hadhi mwenyewe bila kujua.
Leo ni mazungumzo, kesho ni mazoea, kesho kutwa ni fedheha. Jamii haikufundisha kuwa karibu na mkwe kwa namna hiyo, na mila hazikukusudia mkwe awe mtu wa kukaa naye kana kwamba ni rika lako.
Ukivuka mipaka, lawama ya kwanza si mkwe, ni wewe kwa sababu wewe ndiye mwanamume na ndiye uliyetakiwa kusimamia maadili.
Zaidi ya hapo, kuitegemea sapoti ya mkwe badala ya kupambana kutafuta maisha ni aibu kubwa kwa mwanamume mzima.
Msaada wa wazazi au wakwe unatakiwa uwe wa mpito, si nguzo ya maisha yako.
Pale unapofanya sapoti kuwa msingi wa kuendesha familia yako, unajifunga minyororo ya utegemezi na unawapa wengine mamlaka juu ya maamuzi yako.
Ndiyo maana mtu anayekusaidia anaweza kukukalia kooni, kukudharau au kukuvuka mipaka, kwa sababu anajua huna pa kukimbilia
Mwanamume halisi anajengwa na tabu, si starehe. Anajengwa na juhudi, si misaada ya kudumu.
Afadhali kula kwa tabu lakini kwa heshima kuliko kula kwa wingi huku utu wako ukiondolewa makusudi.
Unaposhindwa kupambana kutafuta maisha na badala yake unajificha nyuma ya sapoti ya mkwe, unaua ndoto zako, unadhoofisha sauti yako na unaharibu mfano wako kwa mke na watoto wako.
Watoto hawajifunzi maneno, hujifunza matendo.
Sapoti inayokufanya ushindwe kusema hapana si baraka, ni mtego.
Urafiki unaokuvua heshima si ukaribu, ni hatari. Kama kijana, simama, jitegemee, pambana, hata kama ni hatua ndogondogo.
Weka mipaka kwa mkwe, heshimu nafasi yake, na heshimu nafasi yako kama mwanamume.
Kuanzia leo weka mipaka, usiruhusu mazungumzo yasiyo na tija kati yako na mkweo, utaushinda huu mtihani bila kumwambia hapana.