Profesa Shemdoe, ataka watendaji kuacha mazoea

Geita. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, amewapa wakuu wa mikoa siku 14 kuunda kamati za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na kuwasilisha madokezo yanayoonyesha miradi mipya iliyobuniwa kupitia fedha ambazo matumizi yake yameonekana kutokuwa ya lazima.

Agizo hilo limetolewa kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyoyatoa Ijumaa Januari 23, 2026 jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa meli mpya ya New MV Mwanza, akisisitiza watendaji wa Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Akizungumza Jumamosi Januari 24, 2026 katika kikao cha ndani kilichowakutanisha watendaji wa idara mbalimbali za Serikali kilichofanyika Manispaa ya Geita, Profesa Shemdoe amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea yanayorudisha nyuma kasi ya utekelezaji wa miradi.

Amesema baadhi ya watendaji wamekuwa na tabia ya kutofuatilia miradi kwa wakati, wakisubiri ziara za viongozi wa juu, hali inayosababisha miradi mingine kuharibika kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Tusisubiri kusikia mradi umeharibika ndiyo twende. Tujiwekee utaratibu wa kutembelea miradi mara kwa mara. Tukikuta sehemu haijatekelezwa vizuri, tuchukue hatua mapema,” amesema Profesa Shemdoe.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Grace Kingalame akizungumza katika Kikao cha Watumishi kilichoongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi



Kwa niaba ya wakuu wa mikoa nchini, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Grace Kingalame, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, ameahidi kuyafikisha maagizo hayo kwa wahusika wote ili yaanze kufanyiwa kazi.

“Tunakushukuru Mheshimiwa Waziri, tunapokea maagizo yako na tunaahidi kuyatekeleza kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa,” amesema Kingalame.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi, amesema Manispaa hiyo itaendelea kusimamia miradi ya Serikali sambamba na kuongeza ukusanyaji wa mapato, akisema katika mwaka wa fedha 2025/26 wamejipanga kukusanya zaidi ya Sh22 bilioni na tayari wamefikia asilimia 64 ya lengo hilo.

Kando na kikao hicho, Profesa Shemdoe amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya kilomita 18 inayounganisha wilaya za Nyang’wale na Geita, mradi unaotarajiwa kuwa mkombozi kwa wananchi wa maeneo hayo.

Barabara hiyo inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini (Tarura), ilianza kutekelezwa Agosti 25, 2025 na inatarajiwa kukamilika Februari 27, 2026 kwa gharama ya Sh1 bilioni, ikijengwa na mkandarasi mzawa, Madata Investment Limited, ambapo hadi sasa imefikia asilimia 82 ya utekelezaji.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi tisa inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mpango wa CERC–DMDP awamu ya pili, inayotekelezwa mkoani Geita katika wilaya za Geita, Mbogwe na Chato, yenye thamani ya Sh4 bilioni.