Sakata la Musukuma, mwekezaji, Serikali yatoa maagizo

Geita. Serikali imetoa siku 14 kutafutwa na kupatikana ufumbuzi wa mgogoro kati ya Kamati ya Uchumi na Fedha ya Halmashauri ya Manipaa ya Geita na mwekezaji wa majengo ya biashara, Rashid Kwanzibwa.

Mgogoro huo umeibuka baada ya kamati hiyo kukuta mwekezaji huyo amebomoa baadhi ya majengo ya Serikali yaliyoko eneo la uwanja wa mpira wa miguu, bila kibali cha halmashauri.

Kipande cha picha jongefu kilichosambaa katika mitandao ya kijamii tangu jana, kinamwonesha mwekezaji huyo akirushiana maneno na Mbunge wa Geita, Joseph Musukuma.

Katika picha jongefu hiyo, mwekezaji huyo amesikika akigoma kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa na Musukuma kuhusu uhalali wa uwekezaji wake, akidai hawezi kujibu kwa kuwa aliyesaini naye mkataba ni Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Mimi nimefunga mkataba na wewe? Nikuoneshe mkataba wa nini? Ukitaka mkataba si nenda mahakamani, mimi ni mwekezaji sina sababu za kuzungumza na ninyi hapa sio eneo la Serikali,” amesikika Kwanzibwa akizungumza.

Inadaiwa Kwanzibwa aliingia mkataba wa uwekezaji wa ujenzi wa majengo ya biashara eneo la wazi linalomilikiwa na CCM katika Mtaa wa Katoro CCM.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa, amekiuka kanuni za kimkataba baada ya kuvunja majengo manne yanayomilikiwa na CCM Katoro bila kufuata utaratibu.

Kufuatia sakata hilo, jana Jumamosi Januari 24, 2026, Waziri wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe ametoa agizo alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya shule, barabara na kituo cha afya mkoani Geita.

Amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Geita (Martin Shigella), kufuatilia ili kujiridhisha ikiwa mwekezaji huyo ana mkataba na ikibainika hana, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

“Pale Katoro, mkurugenzi uko hapa, kuna mbabe mmoja amechukua eneo la Serikali, amevunja majengo yaliyopo katika eneo la Serikali, ameanzisha biashara pale, anapozungumza na viongozi wa Serikali anawadharau maana yake ni mbabe amewaweka viongozi mfukoni,” amesema Profesa Shemdoe.

Ametaka mwekezaji huyo apelekewe taarifa za waziri kupitia vyombo vilivyopo na kwamba, wafuatilie.

“Hatua za kisheria zichukuliwe, nimeona ile clip inaendelea kuzunguka haijanibariki kabisa na nipate mrejesho ndani ya siku 14 kwamba suala hili limesimama kwenye msimamo upi, Serikali haiwezi kuchezewa hata kama una fedha,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Katibu wa Siasa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Geita, Emmanuel Mnenke amesema baada ya kuona kinachoendelea katika mitandao, uongozi wa chama umekutana leo kupitia Kamati ya Siasa ya Mkoa.

Amesema katika kikao hicho kamati itapitia mikataba ya mwekezaji huyo.

“Tumeona kinachoendelea mitandaoni, lakini kamati ya siasa ya mkoa tumeitisha kikao kwa kuwa sio wajumbe wote watakuwa wameona kinachoendelea, tumeomba nakala zote za mikataba kutoka CCM Wilaya, tunakwenda kupitia mikataba ili kujiridhisha na tutakuja na majibu rasmi,” amesema Mnenke.