Unguja. Ili kutatua changamoto za wananchi katika kufuata huduma za matibabu, Sh30.44 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Itakapokamilika, hospitali hiyo itapunguza gharama za kufuata huduma za matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Lumumba, au nje ya Zanzibar.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Wizara ya Afya kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi huo na Kampuni ya Cross World Construction Limited.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Kaskazini Unguja una jumla ya wakazi 257,000, ukiwa wa pili kwa idadi kubwa ya watu baada ya Mkoa wa Mjini Magharibi. Mbali na wingi wa watu, pia mkoa huo unaongoza kwa uwekezaji mkubwa wa hoteli nyingi za kitalii huku ukiwa wa pili kwa kuchangia pato la taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo leo, Jumapili, Januari 25, 2026, Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, amesema ujenzi wa hospitali hiyo utatatua changamoto za upatikanaji wa huduma za afya siyo tu katika mkoa huo bali Zanzibar kwa ujumla.
“Mradi huu utakuwa ni faraja na ufumbuzi wa upatikanaji wa huduma za kibingwa za afya kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa yote ya Zanzibar,” amesema kaimu waziri huyo.
Pia amesema ujenzi wa mradi huo utaipunguzia gharama Serikali ya kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuhakikisha wanatibiwa hapa hapa Zanzibar.
Amesema Serikali, kupitia Wizara ya Afya, itaendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa hospitali hiyo ili kuhakikisha vigezo na viwango vya kimataifa vya ujenzi vinavyotakiwa vinafikiwa, na kuona mradi huo unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mngereza Mzee Miraji, akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu mradi huo, amesema katika kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa nchini, Serikali inaendelea kujenga hospitali kubwa za mikoa katika maeneo mbalimbali ili kutimiza azma yake.
Amesema hospitali hiyo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja itakuwa na ghorofa tano, vitanda 200 na kutoa huduma mbalimbali za kibingwa za kimkoa.
Dk Mngereza amefahamisha kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja ni wa kimkakati kutokana na hadhi yake katika shughuli za kitalii, hivyo hospitali hiyo itazingatia huduma zote muhimu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Cross World Construction Limited, Himidi Iddi Mgeni, amesema kampuni hiyo ni ya wazawa na imeshatekeleza miradi mbalimbali mikubwa na midogo katika mikoa mingi ya Tanzania Bara.
Amebainisha kuwa mradi huo ni wa miezi 18, lakini wanatarajia kuukamilisha kabla ya miezi 16 ili kutimiza azma ya Serikali ya kuwafikishia wananchi huduma za matibabu karibu na mikoa yao na kupunguza msongamano katika hospitali za rufaa.
“Wataalamu wapo na vifaa vya kutosha, hivyo hakuna jambo litakalochelewesha kukamilisha mradi huo kwa wakati,” amesema.
Baada ya kukamilika hospitali hiyo, ambayo kwa mujibu wa mkataba ujenzi wake ni wa miezi 18, itakuwa ndiyo hospitali ya kwanza kubwa kwa Zanzibar.