Dar es Salaam. Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema mke wake ameshambuliwa na vikosi vya ulinzi vilivyovamia nyumbani kwake wakati yeye akiwa mafichoni, tukio lililoongeza sintofahamu ya kiusalama nchini humo.
Kupitia taarifa aliyochapisha mtandaoni, Wine amesema shambulio hilo lilitokea Jumamosi Januari 24, 2026, ambapo askari waliovalia kiraia walimshambulia mke wake wakimtaka afichue mahali alipojificha mumewe.
Amesema mke wake alikabwa koo, kuzuiwa chini ya mtutu wa bunduki na baadaye kukimbizwa hospitali ambako bado amelazwa akipatiwa matibabu ya majeraha ya mwili na msongo wa kisaikolojia.
“Walivamia nyumba yangu nikiwa sipo, wakapora mali na kumshambulia mke wangu wakimtaka aseme nilipo,” ameandika Wine kwenye ukurasa wake wa X.
Wine yupo mafichoni tangu baada ya uchaguzi wa Januari 15, 2026, matokeo ambayo ameyakataa akisema hayakuakisi matakwa ya wananchi.
Tukio hilo linajiri siku chache baada ya Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Muhoozi Kainerugaba, kumtaka Wine ajisalimishe Polisi ndani ya saa 48, akimtishia kumchukulia kama mhalifu au muasi endapo hatatii agizo hilo.
Hata hivyo, Wine alikataa agizo hilo akisema yeye si mhalifu bali ni mgombea urais, akisisitiza kuwa kugombea urais si kosa.
Katika ujumbe mwingine ulioibua wasiwasi zaidi, Kainerugaba aliandika mtandaoni akidai Jeshi limewaua makada kadhaa wa Chama cha National Unity Platform (NUP) na kuwakamata mamia, likiwataja kama magaidi.
Kauli hizo zimekosolewa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu na wachambuzi wa siasa nchini Uganda, wakisema zinadhoofisha misingi ya demokrasia.
Kufuatia hali hiyo, mwanasheria wa Bobi Wine, Robert Amsterdam, ameutaka Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kushinikiza kuhakikishwa kwa usalama wa mwanasiasa huyo na familia yake.
“Bobi Wine hajafanya kosa lolote. Tatizo lake ni kuikosoa serikali kwa njia ya amani na kutumia haki zake za msingi,” amesema Amsterdam.
Umoja wa Ulaya na mashirika ya haki za binadamu pia yameeleza wasiwasi kuhusu hali ya amani nchini Uganda, yakitaja vitisho, ukandamizaji na mashambulizi dhidi ya viongozi na wafuasi wa upinzani baada ya uchaguzi.