Tathimini yafanyika kutatua kero ya barabara Uyole

Mbeya. Kilio cha barabara na huduma nyingine za kijamii katika Kata ya Uyole huenda kikaisha baada ya Serikali kufanya tathimini kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi, huku wananchi wakipongeza hatua hiyo.

Uyole ni moja ya kata 13 inayounda jimbo jipya la Uyole ikidaiwa kutokuwa na baadhi ya huduma za kijamii ikiwa ni kituo cha afya, zahanati wala hospitali, kituo cha Polisi, ubovu wa barabara, kero ya maji na kufanya wananchi kufuata huduma hizo sehemu nyingine.

Akizungumza leo Januari 25 wakati akikagua miundombinu ya barabara inayounganisha mitaa ya Utukuyu na Ibala yenye urefu wa kilomita 4.5, Diwani wa Kata hiyo, Benjamin Mwandete amesema changamoto zinazowakabili wananchi zipo katika utekelezaji.

Amekiri kuwa kata hiyo ambayo ndio inabeba taswira ya jimbo, haina kituo cha Polisi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao, huduma ya afya na hakuna barabara yoyote yenye kiwango cha lami, akibainisha kuwa tayari Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi wameanza utekelezaji.

Diwani wa Kata ya Uyole, Benjamin Mwandete akionesha barabara inayounganisha mitaa ya Utukuyu na Ibala yenye urefu wa kilomita 4.5 ambayo imekuwa kero. Picha na Sadam Sadick



“Barabara hii ni kero sana, lakini wiki iliyopita nilikutana na Meneja wa Tarura (Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini )akaja kufanya tathmini na wiki ijayo tunatarajia ujenzi kuanza, lakini sijaishia hapo, zipo hatua kadhaa nimechukua.”

“Kwa nafasi ya udiwani nitawasilisha kero na kufuatilia utekelezaji wake, lakini hata kabla ya kuchukua nafasi hii nilishachimba visima kwa ajili ya huduma ya maji kusaidia wananchi, kuunga mkono ujenzi wa madaraja kwenye mitaa ikiwamo kwa Wachina,” amesema Mwandete.

Amisa Mussa mkazi wa Uyole ya Kati, amesema barabara na afya ni moja ya changamoto na kero kubwa katika kata hiyo, akieleza kuwa hatua za Serikali kufanya tathmini katika maeneo hayo yanarejesha matumaini mapya.

Naye John Mwasika amesema wana matumaini na uongozi uliopo sasa kwa kuwa diwani na mbunge wote wana uzoefu katika masuala ya utendaji kijamii, akiomba wananchi kutoa ushirikiano wanapohitajika.