Trident FC, Mourice Sichone ngoma ngumu

BADO hali haijawa shwari kwa kinda wa Kitanzania, Mourice Sichone na klabu anayoitumikia Trident FC ya Zambia ambao wanadai hawako tayari kumuachia kwa sasa hadi mkataba wake utakapotamatika.

Kinda huyo (18) alisajiliwa dirisha dogo msimu uliopita akitokea Mpulungu Harbour FC ya nchini humo alikocheza mechi 12 na kuhusika katika mabao tisa akifunga manne na kuasisti matano.

Iko hivi, kinda huyo amebakiza mkataba wa miezi mitatu na chama hilo linaelezwa bado linamhitaji hadi mkataba wake utakapomalizika.

Sichone alipata ofa kutoka timu mbalimbali za Ligi Kuu ikiwemo Namungo ambayo iko tayari kumnunua baada ya kuona uwezo wake alipofanya majaribio ya mwezi mmoja.

Kwa kuwa alikuwa na mkataba Namungo iliwafuata Trident na kuwapelekea ofa ya kumtaka lakini walirudisha majibu kuwa bado wanamhitaji.

Mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo aliliambia Mwanaspoti; “Wanataka kumshawishi abaki kule lakini mchezaji mwenyewe hataki kutokana na changamoto za nje ya uwanja alizokutana nazo, hata ile ofa sio kwamba hawaitaki lakini bado wanamhitaji.”