Dar es Salaam. Uamuzi wa Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 wa kuzuia waandishi wa habari kushuhudia vikao vya kupokea ushahidi wa waathirika, umeibua mjadala miongoni mwa wanasheria, wataalamu wa afya ya akili, wanahabari na watetezi wa haki za binadamu, huku wengine wakiunga mkono hatua hiyo na wengine wakipinga.
Wanaounga mkono uamuzi huo wanasema ni muhimu kulinda faragha na afya ya akili ya waathirika, wakisisitiza kuwa, si kila taarifa inayotolewa mbele ya tume inapaswa kuenezwa hadharani kabla ya uchunguzi kukamilika.
Kwa upande mwingine, wanaopinga wanasema hatua hiyo inaleta taswira hasi kwa mchakato wa uwazi na maridhiano ya kitaifa, wakibainisha kuwa matukio ya Oktoba 29, 2025 tayari yanafahamika kwa kiasi kikubwa.
Mjadala huo umeibuka jana Jumamosi, Januari 24, 2026, baada ya mjumbe wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu, Ibrahimu Juma kutoa maelekezo kwa waandishi wa habari waliokuwa wamefika Ubungo jijini Dar es Salaam kufuatilia vikao vya kusikiliza waathirika.
“Tunapoanza kupokea ushahidi, waandishi wa habari wote mtatakiwa kutupisha ili kuwapa faragha watoa ushahidi na kulinda ushahidi wao. Baada ya kukamilisha zoezi hilo, mtarejea na mtaweza kuuliza maswali ili kupata taarifa mnazohitaji,” amesema Jaji Juma.
Amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya tume kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya waathirika, waliodai kuwa taarifa zao binafsi zinasambazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii baada ya kutoa ushuhuda wao.
“Tayari tumepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya watoa ushahidi waliodai kuwa taarifa walizotoa ni za binafsi na hawakupenda kuona zikitangazwa hadharani,” amesema Jaji Jum.
Akizungumzia uamuzi huo leo Jumapili, Januari 25, 2026 alipozungumza na Mwananchi kwa simu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi mstaafu wa Polisi (SACP), Jamal Rwambow amesema si sahihi kwa maelezo yanayotolewa ndani ya tume ya uchunguzi kuanza kusambazwa hadharani kabla ya kukamilisha majukumu yake ndani ya siku 90 ilizopewa.
Amesema endapo awali kulikuwa na ruhusa ya maelezo hayo kuenezwa, huenda ilitolewa kimakosa, lakini kuzuia kwake ni hatua iliyo sahihi.
“Naona si sahihi taarifa za ndani ya tume kusambazwa mapema. Kama kulikuwepo ruksa basi ilitolewa kimakosa, lakini kama sasa imezuiwa, basi tume iko kwenye mstari sahihi,” amesema Rwambow.
Hata hivyo, amesema kuzuia waandishi wa habari pekee hakutoshi, akisisitiza kuwa hata watoa ushahidi hawapaswi kuzungumza na mtu mwingine yeyote kuhusu maelezo waliyoyatoa mbele ya tume.
Amesema maelezo yote yanayotolewa ndani ya tume ni mali ya tume na yanapaswa kubaki huko hadi yatakapofanyiwa kazi na kuwasilishwa rasmi.
Rwambow pia amekosoa utaratibu wa kuwakusanya waathirika wengi katika ukumbi mmoja na kuwahoji mmoja baada ya mwingine mbele ya hadhira, akisema hauzingatii faragha wala hauna tija.
“Kila mwathirika anapaswa kupewa nafasi ya kuzungumza peke yake mbele ya tume. Mfumo wa kuwa na watu wengi wakimsikiliza mmoja si mzuri,” amesema.
Akizungumzia hoja hiyo, Mtaalamu wa Saikolojia na Afya ya Akili, Ramadhan Masenga amesema uamuzi wa tume ni wa busara kwa kuwa waathirika wengi bado wanakabiliwa na msongo wa mawazo baada ya kupitia matukio ya kikatili.
“Mtu aliyeshuhudia mauaji au aliyekuwa katika hatari ya kuuawa hubeba maumivu ya kisaikolojia kwa muda mrefu. Wanapaswa kupewa mazingira salama ya kueleza yaliyowapata bila kuhofia unyanyapaa au kuumizwa zaidi,” amesema.
Masenga amesema kuwa kuhojiwa mara kwa mara na waandishi wa habari kunaweza kuwasababishia waathirika kurejea kumbukumbu zenye maumivu, hali inayoweza kudhuru afya zao za akili.
Kwa upande wa wanaopinga uamuzi huo, Wakili Ibrahim Bendera amesema hatua ya kuzuia waandishi wa habari inaleta wasiwasi kwa jamii.
“Hii inaleta picha kwamba tume haitaki jamii isikie yanayosemwa na waathirika jambo linaloweza kuibua hofu kuhusu uhalisia wa matokeo ya uchunguzi,” amesema.
Mtazamo huo umeungwa mkono na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba ambaye amesema uwazi ni jambo muhimu katika mchakato wa uponyaji na maridhiano ya kitaifa.
Amesema ni vigumu kwa jamii kuamini matokeo ya uchunguzi endapo ushuhuda wote unatolewa gizani, akirejea mfano wa Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini iliyofanya kazi zake kwa uwazi.
“Tunataka tupone kama Taifa, na hilo haliwezekani bila ukweli kuonekana wazi. Uwajibikaji unahitaji uwazi,” amesema.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA-TAN), Edwin Soko amesema hakubaliani na uamuzi wa tume, akisema unadhoofisha dhana ya tume huru na uwazi katika mchakato wa kutafuta maridhiano.
“Ukweli ndiyo msingi wa haki. Kauli za waathirika ndizo zinazoonesha tulipokosea na nini kifanyike ili taifa lipone,” amesema.
Hata hivyo, tume imesisitiza kuwa lengo lake ni kufanya kazi kwa umakini na weledi, ikiwataka Watanzania kutoa muda ili itimize wajibu wake kabla ya kuhukumiwa.