Dar es Salaam. Kundi la wanafunzi zaidi ya 190 kutoka nchini Sudan waliokuwa wanasoma udaktari Tanzania wamehitimu masomo yao na kushukuru kwa ukarimu walioupata.
Wanafunzi hao wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Matibabu (UMST), walikwenda nchini Tanzania miaka miwili iliyopita baada ya kukumbwa na vita nchini kwao, walikuwa wakisoma huku wakipata mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Akizungumza kwenye mahafali ya wanafunzi hao yaliyofanyika usiku wa kuamkia leo Jumapili, Januari 25, 2026, jijini Dar es Salaam, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka MNH, Verdiana Byemelwa amesema wageni hao wamekuwa wakipata mafunzo Muhimbili kwa muda wote waliokuwa nchini.
“Udaktari hauishi tu kwa kusoma darasani bali kuna mafunzo kwa vitendo na wamekuwa wakiyapata Muhimbili. Kama taifa na hospitali tuliwapokea waendelee na mafunzo baada ya kupata changamoto nchini kwao,” amesema.
Wanafunzi wa chuo kikuu cha (UMST) kutoka nchini Sudan waliokuwa wakisoma udaktari Tanzania wakiwa kwenye mahafali yaliyofanyika usiku wa kuamkia Jumapili Januari 25, 2026 Dar es Salaam mara baada ya kuhitimu.
Hata hivyo, Tanzania imekuwa ikipokea wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini wanaosomea mafunzo kwa vitendo.
Profesa wa tiba, Mamoun Homeida wa UMST amesema anashukuru kwa ukarimu walioupata kwa kumalizia kuwafundisha wanafunzi hao huku akiahidi ushirikiano zaidi na Tanzania.
“Tulianza Sudan lakini tumemalizia Tanzania kwa sababu ya vita. Ningependa kuwapongeza wahitimu wote na kipekee kuwashukuru Watanzania pamoja na mazingira mazuri, ambapo imekuwa msaada mkubwa katika kuwahudumia wanafunzi wetu katika Chuo Kikuu cha Muhimbili,” amesema.
Amesema wameridhika na kila kitu walichokikuta Tanzania. Amedokeza kwamba UMST sasa kitaanzishwa Tanzania kinachosubiriwa ni taratibu za usajili.
Mmoja wa wahitimu hao, Qutb Osama Elhag amesema walianza Sudan lakini kwa bahati mbaya wakasimama kimasomo kutokana na vita na wamekuja kumalizia Tanzania.
“Watanzania ni wazuri sana na wakarimu kwetu. Tumekaa hapa, kama miaka miwili, na leo ndiyo siku yetu ya mwisho. Tunafanya mahafali yetu, tunawapenda Watanzania,” amesema.
Kwa upande wake, Sara Omer amesema mazingira ya Tanzania yamewafanya wajihisi wako nyumbani kwa sababu ya usalama na utulivu.
Wanafunzi wa chuo kikuu cha (UMST) kutoka nchini Sudan waliokuwa wakisoma udaktari Tanzania wakiwa kwenye mahafali yaliyofanyika usiku wa kuamkia Jumapili Januari 25, 2026 Dar es Salaam mara baada ya kuhitimu.
“Elimu nchini Tanzania ni nzuri ninatamani nifanye kazi au kufanya mafunzo yoyote ya hiari nchini Tanzania ila kwa sasa narudi nchini mwangu,” amesema.