Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wateja wakilalama kuhusu kuisha haraka kwa umeme wanaonunua kupitia mfumo wa Luku, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema hakuna jibu la moja kwa moja bila kufanyika tathmini ya kitaalamu.
Kwa mujibu wa waliotoa malalamiko, wamekuwa wakinunua umeme kiwango kilekile lakini huisha ndani ya muda mfupi licha ya kuwa hawajaongeza matumizi ya nishati hiyo.
Akizungumza na Mwananchi Ijumaa Januari 23, 2026, Halman Fred, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, amesema nyumbani kwake ana jokofu, pasi na feni na amekuwa akitumia umeme wa Sh10,000 kwa siku saba lakini sasa unatumika siku nne pekee.
Amesema alihoji hali hiyo kupitia kundi zogozi la Tanesco (WhatsApp) akajibiwa aangalie kama umeme unavuja mahali.
“Nikamwambia yule ofisa nimefanya vyote hivyo kwa kuzima vitu vyote na kwenda kazini, niliacha uniti 13.33 lakini niliporudi nilikuta uniti 12.39,” amesema.
Amesema bajeti imeongezeka kutoka Sh40,000 kwa mwezi na kufikia Sh70,000 kwa ajili ya matumizi ya umeme.
Kwa upande wake, Malaika Tiba, mkazi wa Sinza, amesema alikuwa akitumia umeme wa Sh20,000 kwa mwezi kwa matumizi ya jokofu, runinga na pasi, ambayo haitumii mara kwa mara, lakini kwa sasa kiasi hicho hakimalizi wiki mbili.
Mteja aliyejitambulisha Mary Rose, mkazi wa Magomeni, amesema: “Nilijua ni mimi peke yangu, nilifika hadi ofisi za Tanesco nikaomba fundi aje kukagua. Alikagua na kuniambia kila kitu kiko sawa cha kushangaza, bado umeme unaendelea kuisha haraka. Uniti 126 haziwezi kumaliza mwezi ilhali matumizi ni ya kawaida kabisa ya nyumbani,” amesema.
Kwa upande wake, Juliana Wandiba, wenye ofisi ndogo ya kuchapa nakala na kutengeneza logo mbalimbali amesema:
“Ofisini tuna feni, taa na kompyuta tu, lakini umeme wa Sh10,000 unaisha ndani ya siku mbili. Nilinunua tokeni yenye uniti 28 Januari 16, lakini ifikapo Januari 18 ulikuwa umekatika.”
Lazaro Nicholaus, mkazi wa Kinyerezi amesema anatumia umeme wa Sh10,000 kwa mwezi akipata uniti 28 au 23.8 iwapo kuna makato. Nishati hiyo huitumia kuwasha taa na runinga pekee, lakini sasa anatumia wiki mbili tu kwa matumizi yale yale.
“Nimenunua umeme Januari 9, 2026 nikapata uniti 23.8 na Januari 23, 2026 nimenunua nikapata uniti 28. Umeme ambao nilikuwa nakaa nao siku 28 hadi 30 nikakaa nao siku 14 hadi 15 na matumizi yangu ni runinga na taa pekee sina kitu cha ziada, pasi naweza kutumia mara moja kwa wiki,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Januari 23, 2026 Mkurugenzi wa Tanesco, Lazaro Twange, amesema hakuna jibu la moja kwa moja linaloweza kutolewa bila kufanya tathmini ya kitaalamu katika eneo husika.
Amesema mara nyingi changamoto hiyo husababishwa na miundombinu ya ndani ya nyumba, ambayo haiko chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Tanesco.
“Hatuna jibu la moja kwa moja kusema tatizo ni hili au lile, kwa sababu umeme unapoingia nyumbani, miundombinu ya ndani inasimamiwa na mmiliki wa nyumba kwa kushirikiana na mkandarasi wake,” amesema.
Twange amesema hatua ya kwanza kwa mwananchi anayekumbwa na tatizo hilo ni kumtafuta fundi au mkandarasi aliyemtengenezea mifumo ya umeme ili akague kama mfumo wa ndani uko sawa.
“Baada ya mkandarasi kukagua na kubaini kuwa miundombinu iko sawa, basi Tanesco tunaweza kushirikiana na kumpelekea timu ya wataalamu kufanya tathmini zaidi,” amesema.
Amesema sababu nyingine ya umeme kuisha haraka ni wizi au miunganiko haramu, akieleza baadhi ya watu hujiunganishia umeme bila ridhaa ya mmiliki wa mita.
“Unaweza kwenda kazini, hujui kinachoendelea nyumbani. Kuna mtu amejiunganishia umeme wako bila wewe kujua na hilo linaathiri matumizi yako,” amesema.
Amesema kutokana na sababu hizo kuwa nyingi na tofauti ni lazima kufanyika uchunguzi wa kina kabla ya kubaini chanzo halisi cha tatizo.
Hata hivyo, amesema Tanesco iko tayari kushirikiana na wananchi kwa kutoa msaada wa kitaalamu pale wanapopata taarifa za moja kwa moja kutoka kwa wateja wanaolalamika.
“Kama kuna mteja mmoja au zaidi tunamfahamu na ana malalamiko haya, tusaidieni kumpata ili tupeleke timu ya kiufundi ikafanye tathmini na kutoa suluhisho,” amesema.
Amesema taarifa za malalamiko hayo zitafikishwa kwa mameneja wa mikoa na wilaya ili kubaini kama ni changamoto inayojirudia katika maeneo mbalimbali.