Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kusikitishwa na taarifa ya Marekani kujiondoa katika shirika hilo, uamuzi unaoelezwa kuifanya Marekani na dunia kwa jumla kuwa katika hatari zaidi.
Januari 20, 2025, Rais wa Marekani Donald Trump alitoa notisi ya kujiondoa WHO kupitia amri ya utendaji, kabla ya nchi hiyo kujitoa rasmi Januari 22, 2026. Marekani ilisema inapanga kufanya kazi moja kwa moja na nchi nyingine badala ya kupitia mashirika ya kimataifa katika ufuatiliaji wa magonjwa na vipaumbele vingine vya afya ya umma.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya kujiondoa iliyolifikia shirika hilo, Alhamisi Januari 22, 2026 inaibua masuala yatakayojadiliwa na Bodi ya Utendaji ya WHO katika kikao chake cha kawaida kitakachoanza Februari 2, 2026 na pia Mkutano wa Afya Duniani wa Mei 2026.
WHO imetoa kauli hiyo jana Jumamosi, Januari 24, 2026 iliyozingatia kauli za Serikali ya Marekani zinazodai WHO, imeharibu na kuchafua heshima yake, imeitukana na kuhatarisha uhuru wake.
Imeeleza kuwa, kinyume chake ndicho kilicho kweli. Kama ilivyo kwa kila nchi mwanachama, WHO imekuwa ikijitahidi kushirikiana na Marekani kwa nia njema, kwa heshima kamili ya mamlaka na uhuru wake wa kitaifa.
Katika kauli zake, Marekani imetaja miongoni mwa sababu za uamuzi wake ni kwa kile ilichokiita upungufu wa WHO wakati wa janga la Uviko-19, ikiwamo kuzuia ushirikishwaji kwa wakati na kwa usahihi wa taarifa muhimu.
Ingawa hakuna shirika wala Serikali iliyofanya kila jambo kwa ukamilifu, WHO imesema inasimamia msimamo wake kuhusu mwitikio wake katika janga hilo lisilo la kawaida la kimataifa.
“WHO ilipendekeza matumizi ya barakoa, chanjo na umbali wa kimwili, lakini haikuwahi kupendekeza maagizo ya lazima ya barakoa, chanjo au kufunga shughuli (lockdowns). Tulizisaidia Serikali huru kufanya uamuzi walioona una masilahi mapana ya watu wao.
“Baada ya kupokea taarifa za awali za kundi la wagonjwa wa imonia ya chanzo kisichojulikana, mjini Wuhan, China, Desemba 31, 2019, WHO iliomba taarifa zaidi kutoka China na kuanzisha mfumo wake wa usimamizi wa matukio ya dharura,” inaeleza taarifa hiyo.
“Kufikia wakati kifo cha kwanza kilipotangazwa kutoka China Januari 11 2020, WHO ilikuwa tayari imeitaarifu dunia kupitia njia rasmi, taarifa za umma na mitandao ya kijamii, imewakutanisha wataalamu wa kimataifa, na kuchapisha mwongozo wa kina kwa nchi kuhusu jinsi ya kulinda watu wao na mifumo yao ya afya.”
Kiwango cha juu kabisa cha tahadhari chini ya sheria za afya za kimataifa nje ya China kilikuwa chini ya kesi 100 zilizoripotiwa na hakuna kifo kilichoripotiwa.
WHO imesema katika wiki na miezi ya mwanzo ya janga, mkurugenzi mkuu aliyaonya mara kwa mara mataifa yote kuchukua hatua za haraka kulinda watu wao, akisisitiza dirisha la fursa linazidi kufungwa.
“Kufuatia tathmini mbalimbali za janga la Uviko-19, zikiwamo zile zilizochunguza utendaji, WHO imechukua hatua za kuimarisha kazi zake na kusaidia nchi kuimarisha uwezo wao wa maandalizi na mwitikio dhidi ya majanga.
“Mifumo tuliyoanzisha na kuisimamia kabla, wakati na baada ya awamu ya dharura ya janga, na ambayo inafanya kazi saa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki, imechangia kulinda usalama wa nchi zote, ikiwemo Marekani,” inaeleza taarifa hiyo.
Imefafanua kuwa, Marekani pia ilisema katika kauli zake kwamba WHO imefuata ajenda ya kisiasa inayochochewa na mataifa yanayopingana na masilahi ya Marekani, dai lililotajwa kuwa si la kweli.
“Kama shirika maalumu la Umoja wa Mataifa, linaloongozwa na nchi wanachama 194, WHO imekuwa na inaendelea kuwa huru na isiyoegemea upande wowote, ikihudumia nchi zote kwa heshima ya mamlaka yao, bila woga wala upendeleo,” inaeleza taarifa hiyo.
WHO imeeleza kuwa, inathamini uungwaji mkono na ushiriki unaoendelea wa nchi wanachama wake wote, wanaoendelea kufanya kazi ndani ya mfumo wa WHO kutafuta suluhisho la vitisho vikubwa vya afya duniani, vya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
Kwa umuhimu mkubwa, nchi wanachama wa WHO mwaka jana walipitisha Mkataba wa Janga la WHO, ambao ukisharidhiwa utakuwa nyenzo muhimu ya kihistoria katika sheria za kimataifa kwa ajili ya kuifanya dunia iwe salama zaidi dhidi ya majanga ya baadaye.
Nchi wanachama kwa sasa zinajadili kiambatisho cha Mkataba wa Janga la WHO, Mfumo wa Upatikanaji na Ugawaji wa Manufaa ya Vimelea ambao ukipitishwa utakuza ugunduzi wa haraka na ushirikishwaji wa vimelea vyenye uwezekano wa kusababisha majanga, pamoja na upatikanaji wa haki na kwa wakati wa chanjo, tiba na vipimo.
Hata hivyo, imeeleza kuwa, ina matumaini kwamba siku zijazo, Marekani itarejea kushiriki kikamilifu katika WHO.
Kwa sasa, WHO inaendelea kufanya kazi na nchi zote katika kutimiza dhamira yake ya msingi na wajibu wake wa kikatiba, kufikia kiwango cha juu kabisa cha afya kinachoweza kupatikana kama haki ya msingi kwa watu wote.
Kama mwanachama mwanzilishi wa WHO, Marekani imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya shirika ikiwamo kutokomeza ugonjwa wa ndui, pamoja na hatua muhimu dhidi ya vitisho vingine vingi vya afya ya umma kama vile polio, VVU, Ebola, mafua, kifua kikuu, malaria, magonjwa yaliyopuuzwa ya kitropiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, usalama wa chakula na mengineyo.