Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Yas imesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imewekeza Sh1 trilioni katika upanuzi na uboreshaji wa miundombinu huku ikichangia mabilioni katika uchumi wa nchi na wananchi.
Mbali na uwekezaji kampuni hiyo imeeleza kuwa imenunua bidhaa na huduma zenye thamani ya Sh569 bilioni kutoka kwa wazabuni wa ndani, Sh418 bilioni kama kamisheni kwa washirika wasio wa moja kwa moja na kuchangia Sh467 bilioni katika kodi mbalimbali, ikiwamo VAT, ushuru wa bidhaa na PAYE.
Akizungumza katika maadhimisho ya mwaka mmoja wa Yas, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo nchini Pierre Bacara amesema uwekezaji huo umewawezesha kuwa na mtandao mpana zaidi wa 4G na 5G, unaowafikia zaidi ya asilimia 95 ya wananchi na kuhudumia wateja milioni 29.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Bacara amesema mbali na huduma za mawasiliano ya simu, Yas pia wamewekeza katika miundombinu ya nyaya ya faiba ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya intaneti ya kasi na ya kuaminika kwa wananchi.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, tumeunganisha zaidi ya nyumba 8,000 jijini Dar es Salaam, tukiziwezesha familia, wataalamu na wafanyabiashara kufanya kazi na kubuni ubunifu kwa kujiamini,” amesema Bacara.
Pia, amesema maandalizi yanaendelea kwa kasi kupanua huduma katika majiji ya Arusha, Dodoma, Mwanza na Zanzibar.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha amesema wamedhamiria kuwa mshirika wa kifedha katika maisha ya Mtanzania kwa kuhakikisha huduma zinakuwa salama, bayana na kuwafikia Watanzania wengi.
“Kila mwezi miamala zaidi ya Sh7trilioni inafanywa na wateja milioni 22, huduma ya lipa kwa simu ina wateja zaidi ya 500,000 na miamala yao kwa mwezi ina thamani ya Sh700 bilioni,” amesema Pesha.
Amesema kupitia huduma zao, mikopo ya Nivushe Plus na Bustisha imewezesha Watanzania milioni 4.8 kupata mikopo ya papo hapo isiyo na dhamana yenye thamani ya Sh1 trilioni ili kukamilisha malengo yao ya kifedha.
Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga ambaye alihudhuria hafla hiyo amesema Yas imeonesha ubunifu unaojikita kwa watu wake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Amesema uwekezaji wao umeboresha mtandao na kuongeza usambazaji jambo ambalo limeongeza upatikanaji wa huduma za kijamii.
“Mtandao umesaidia utoaji wa huduma za Serikali kuwa rahisi, kwani watu wameunganishwa lakini pia huduma hizi zimesaidia kupunguza gharama za utoaji wa huduma na kuongeza urahisi.”
Amesema uwekezaji umetengeneza fursa za ajira kwa wengi na kwa Zanzibar, Yas imesaidia mpango wa Serikali wa kuwa na uchumi wa kidijitali na mpaka sasa visiwani Zanzibar shule 52 zimeunganishwa na mtandao wa intaneti, lakini pia upatikanaji wa huduma za bima kwa wakulima.
Soranga amesema Serikali ya Zanzibar itaendelea kuunga mkono juhudi zinazounga mkono ajenda za nchi na zinazochangia kuboresha maisha ya watu.