Zawadi Usanase anavyoiokoa Simba Queens

MSHAMBULIAJI wa Simba Queens, Zawadi Usanase amekuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya timu hiyo msimu huu baada ya mabao yake muhimu kuiweka kileleni mwa msimamo wa ligi tangu raundi ya kwanza hadi sasa.

Simba iko kileleni na pointi 28, kwenye mechi 10 imeshinda tisa na sare moja ikifunga mabao 21 na kuruhusu mabao mawili.

Usanase aliyesajiliwa msimu huu akitokea Indahangarwa WFC ya Rwanda ameonyesha kiwango kikubwa akibeba matumaini ya wekundu hao wa Msimbazi katika mechi ngumu na zenye presha kubwa, hasa pale timu ilipohitaji pointi tatu au hata moja ili kuendelea kubaki kileleni.

Bao lake la kwanza alifunga dhidi ya Ceasiaa nikiwa ni pekee lililoipa pointi tatu timu hiyo, akafunga tena moja dhidi ya Ruangwa mechi ikiisha kwa Simba kuondoka ikishinda bao 1-0.

Katika mechi ngumu dhidi ya wapinzani wao JKT Queens ambao walikuwa tayari wametangulia kwa bao moja, nyota huyo akasawazisha na mzani kuwa sawa 1-1.

Dhidi ya Mashujaa Usanase akafunga tena mechi iliyomalizika kwa ushindi wa 2-1, bao lililofungwa dakika za jioni na kuwafanya mashabiki wa timu waondoke na pointi zote tatu.

Wiki hii alifunga bao 1-0 dhidi ya Alliance Girls uwanja wa Nyamagana, timu ambayo ilikuwa haijapoteza mechi tano mfululizo nyumbani, lakini rekodi hiyo ikavunjwa na mshambuliaji huyo.

Kwa jumla mabao ya Usanase yamekuwa nguzo muhimu ya Simba msimu huu, yakithibitisha ni mchezaji wa nyakati ngumu ambaye amekuwa akiokoa jahazi na kuiweka Simba kileleni mwa ligi.