DAR ES SALAAM, 26 Januari 2026. Africa Pension Fund Limited (APeF) leo imezindua rasmi Mfuko wa Ziada, ambao ni mfuko wa kwanza wa uwekezaji wa pamoja katika soko la fedha nchini Tanzania unaojumuisha mafao ya bima ya maisha, hatua inayoweka alama muhimu katika kupanua upatikanaji wa suluhisho za uwekezaji zilizo chini ya udhibiti.
Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuriwa na mgeni rasmi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, ikihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), mifuko ya hifadhi ya jamii, wasimamizi wa mifuko, madalali, taasisi za kibenki na bima, pamoja na wanahabari.
Mfuko wa Ziada umebuniwa kuwasaidia wawekezaji kuweka akiba na kukuza fedha zao kupitia uwekezaji wenye nidhamu katika soko la fedha, ukiwa na faida ya ziada ya ulinzi wa bima ya maisha kwa wawekezaji binafsi wanaokidhi vigezo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa APeF, Bw. Mfaume Kimario, alisema, Ziada imeundwa kwa wawekezaji wanaotaka njia rahisi na za kuaminika za kukuza fedha zao bila kupoteza uwezo wa kupata fedha zao pindi zinapohitajika.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti na Bodi ya Wakurugenzi, Dkt. Hamisi Kibola, Mjumbe wa Bodi ya APeF, aliipongeza CMSA kwa hatua zilizofikiwa katika kuendeleza masoko ya mitaji nchini Tanzania na kwa kukuza ukuaji na uhai unaoonekana sokoni kwa sasa.
Mfuko wa Ziada umeandaliwa kwa ushirikiano na taasisi washirika muhimu, ambapo Alliance Life Assurance Limited ni mtoa bima, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ni Mtunza Dhamana na Mdhamini. Wawekezaji wanaweza kupata huduma za Mfuko wa Ziada kupitia benki wakusanyaji zikiwemo CRDB Bank, NMB Bank, Exim Bank, Azania Bank, COOP Bank, NBC na Mwanga Hakika Bank, pamoja na kupitia mawakala walioidhinishwa na DSE na majukwaa ya kidijitali ya APeF.
“Tunaalika Watanzania kufanya suala la kuweka akiba kuwa utamaduni wao kupitia Ziada. Unapoweka akiba kwa uthabiti, unaimarisha familia yako, kuinua jamii yako, na kuunga mkono maendeleo ya taifa. Ziada inakupa mahali rahisi pa kuanzia, kukua hatua kwa hatua, na kulinda kile kilicho muhimu zaidi,” aliongeza Ofisa Mtendaji Mkuu wa APef, Bw. Kimario.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mkama alisema kuidhinishwa kwa mfuko wa ziada kunaendelea kuleta chachu zaidi katika maendeleo ya uwekezaji kwenye mifuko hiyo na kuifanya idadi ya mifuko hiyo ya uwekezaji wa pamoja kufikia 26.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Africa Pension Fund (APeF), Bw. Mfaume Kimario, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Ziada Fund, jijini Dar es Salaam leo.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Africa Pension Fund (APeF), Dkt. Hamisi Kibola akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Ziada Fund, jijini Dar es Salaam leo.

Baadhi ya wadau wakihudhuria hafla ya uzinduzi rasmi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Ziada Fund unaoendeshwa na Africa Pension Fund (APeF).

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Africa Pension Fund (APeF), Bw. Mfaume Kimario (kushoto) akizungumza na baadhi ya wadau wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Ziada Fund wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfuko huo, jijini Dar es Salaam leo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, (CMSA), CPA Nicodemus Mkama (katikati) , Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Africa Pension Fund (APeF), Dkt. Hamisi Kibola ( wa nne kushoto) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa APeF, Bw. Mfaume Kimario ( wa nne kulia ) wakipiga picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo baada uzinduzi rasmi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Ziada Fund, jijini Dar es Salaam leo.
