Dodoma. Mkutano wa pili wa Bunge la Tanzania unaanza kesho Jumanne, Januari 27, 2026 huku mambo matano yakitarajiwa kutokea katika kipindi cha wiki mbili cha mkutano huo.
Ni mkutano utakaoshuhudiwa kwa mara ya kwanza katika Bunge linaloongozwa na Spika Mussa Zungu likiwa na Serikali kamilifu kwa maana ya Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) pamoja na mawaziri wote.
Katika mkutano wa kwanza wa Bunge hilo la 13 ambalo Rais Samia Suluhu Hassan alilizindua Novemba 13, 2025, halikuwa na mawaziri.
AG Hamza Johari alikuwapo na baadaye Dk Mwigulu Nchemba akawa Waziri Mkuu.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujiri katika mkutano huo ni mjadala wa Hotuba ya Rais Samia wakati wa kulizindua Bunge, maswali ya papo kwa hapo kwa mara ya kwanza mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akiwa kwenye cheo hicho kipya.
Katika Bunge la 12, Kassim Majaliwa ndiye alikuwa Waziri Mkuu huku Dk Mwigulu alikuwa Waziri wa Fedha. Maswali ya papo kwa hapo yapo kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Mengine ni viapo vya wabunge wapya wawili, Dk Godwin Mollel wa Siha na Asha Hussein Saleh wa Fuoni wote wa CCM waliochaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Desemba 30, 2025.
Majimbo hayo uchaguzi wake uliahirishwa baada ya miongoni mwa wagombea kufariki dunia.
Jambo la nne ni uthibitisho au uchaguzi wa majina matatu ya wenyeviti wa Bunge. Jana Jumapili, Januari 25, 2026, Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), chini ya uenyekiti wa Rais Samia ilifanya uteuzi wa majina matatu na wanaohitajika ni watatu.
Walioteuliwa ni Deodatus Mwanyika, Cecilia Pareso na Najma Murtaza Giga.
Aidha wote watatu ni wenyeviti wa kamati za Kudumu za Bunge ambapo Mwanyika anaongoza kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo. Pareso yeye ni mwenyekiti wa kamati ya Sheria Ndogo huku Giga akiwa ni mwenyekiti wa kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Bunge la 12 lililoongozwa na Spika Tulia Ackson, Mwanyika na Giga walikuwa wenyeviti wa Bunge huku Pareso alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Baada ya Bunge kuvunjwa alihamia CCM. Ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais.
Tano, katika mkutano huo, kutakuwa na taarifa ya Spika inayohusu vifo vya wabunge wawili waliofariki dunia hivi karibuni. Desemba 11, 2025, Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama alifariki dunia katika Hospitali ya Benjani Mkapa, Dodoma kwa ugonjwa wa moyo.
Mhagama ambaye alikuwa mbunge wa Peramiho kwa miaka 20 tangu mwaka 2005, ni miongoni mwa wabunge waandamizi aliyeshika nafasi za uwaziri kwa kipindi kirefu.
Mwingine ni Halima Idd Nassor, mbunge wa viti maalumu aliyefariki dunia Januari 18, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge, Rais Samia alisisitiza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/50, akilenga taifa jumuishi, ustawi, haki, na kuweka nguvu zaidi kwenye sekta zinazoajiri watu wengi.
Rais alisema nguvu itawekwa kwenye sekta zinazozalisha ajira nyingi, na miradi ya ujenzi wa miundombinu.
Rais Samia aligusia vurugu zilizotolea siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi ambapo aliomba Watanzania kuwa wavumilivu ili aunde tume ambayo itatoa majibu ya kilichotokea jambao ambalo amelikamilisha.
Kwenye hotuba hiyo aliwaahidi Watanzania kuwa Serikali anayoiongoza itaacha tabasamu mara baada ya mhura wake na ahadi ya kuwa karibu na kundi la vijana hata akaunda Wizara.
Mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM), Seleman Kakoso amesema kwenye mkutano huu, akili zaidi itaelekezwa kwenye Hotuba ya Rais kwani kuna mambo mengi ya maagizo na maelekezo kwa Taifa muhimu yakatazamwa.
Kakoso ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu amesema baadhi ya mambo aliyosema Rais Samia muhimu yajadiliwe ni eneo la afya, ajira kwa vijana ikiwemo eneo la wachimbaji wadogo na miundombinu ya kufungua Nchi.
“Wabunge tutajikita maeneo hayo maana yanagusa wananchi moja kwa moja, mfano suala la kuzuia maiti hospitalini,bima ya afya kwa wote,na muhimu miundombinu ikiwamo reli ya mwendo kasi ili tufungue nchi yetu,” amesema Kakoso.
Mmoja wa wabunge wakongwe ambaye amewahi kuwa waziri, ametahadharisha kwenye uchangiaji wabunge akisema, wanapaswa kuwa makini vinginevyo wanaweza kujikuta wanatofautiana na wananchi na ama wanakwenda kinyume na malengo ya Rais.
“Sisi wengine ni wakongwe, ukisimama ukasifia kila kitu lazima uwe kinyume na wapiga kura, lakini ukitaka kukosoa napo ni shida kwa watawala kwa hiyo inabidi mtu usome ili ubebe hoja ambayo haitakujeruhi,” amesema huku akiomba jina lake lisiandikwe.
Mratibu Mkuu wa Umoja wa Wastaafu, Ezekiel Oluoch amesema kwa sasa nchi ‘inaumwa’ lakini inategemea wa kuiponya ambao ni wabunge hu akasisitiza kuwa muhimu wasiwe ‘wanafiki.’
Oluoch ambaye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Mjumbe wa Bunge la Katiba, amedai kuna mpasuko ndani ya Taifa uliotokana na makovu ya uchaguzi mkuu ambayo yameacha malalamiko makubwa.
“Hotuba zitawapambanua, wengi wanalalamikiwa kuwa hawakuchaguliwa, lakini Serikali imetuambia waliokufa walikuwa wachache, sasa maiti zao ziko wapi ili ndugu wakawazike wapendwa wao,” amedai Olouch.
“Lakini jukumu la wabunge kuishauri Serikali ilipe fidia za moja kwa moja wale waliopata madhira lakini wakija na mtindo wa kusifia hotuba itakuwa tatizo,” amesema Oluoch.
Amewataka viongozi kuiga mfano wa Rais wa pili hayati, Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliyejiuzulu wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya mauaji ya watu Shinyanga akisema kuwajibika siyo dhambi na wakuu wa mikoa na Polisi zilikotokea vurugu wabunge wapaze sauti ili wawajibike kabla ya ripoti ya tume ya Kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga amesema mjadala ndani ya Bunge ujikite kwenye kuponya Taifa kwani bado kuna maumivu na watu wanatafuta mahali pa kupumulia lakini hawana.
Dk Henga ametolea mfano wa msiba wa mwasisi wa Chadema na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei kwamba walipopata nafasi watu walitoa ya moyoni, hivyo angetamani wabunge wachonge njia ili kuruhusu mjadala wa Kitaifa katika kutibu alichokiita majeraha makubwa.
“Wabunge wasiingie kwa mfumo wa kutaka sifa za ubora fulani kasema, sisi tunataka waelekeze akili zao kwenye mjadala mpana wa kuondoa maumivu ili watu wafunguke na nyongo watakazotema zisikilizwe,” amesema Dk Henga.
Msiba anaouzungumzia Dk Henga ni wa Mzee Mtei aliyefariki dunia Januari 19, 2026 nyumbani kwake Tengeru, Mkoa wa Arusha.
Siku ya maziko yake Januari 24,2026 viongozi mbalimbali wa kisiasa wa upinzani na Serikali akiwemo Waziri Mkuu, Dk Mwigulu aliyemwakilisha Rais Samia walikuwapo.
Viongozi hao wa kisiasa, walipopata fursa ya kuzungumza walitema nyongo za kuomba uponyaji wa Taifa kutokana na majeraha yaliyotokea na Dk Mwigulu aliahidi kuyachukua na kwenda kuyafanyia kazi serikalini.
