MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema katika kipindi cha miaka mitano, kumekuwa na maendeleo makubwa na ustawi mzuri wa uwekezaji katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
Imefafanua katika kipindi kilichoishia Disemba 2025 imeongezeka kwa asilimia 65.10 na kufikia Sh. trilioni 4.35, ikilinganishwa na Sh. trilioni 2.64 katika kipindi kilichoishia Disemba mwaka 2024 huku ikisisitiza Katika kipindi cha miaka mitano, kumekuwa na maendeleo na ustawi mzuri katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja, ambapo mifuko mipya na bunifu imeanzishwa.
Hayo yameelezwa leo Januari 26,2026 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mkama katika hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Kampuni ya Africa Pension Fund Limited (APEF) unaoitwa Ziada Fund.
“Mifuko hii inatoa fursa kuwekeza kwa kiwango cha chini na hivyo kuvutia wawekezaji wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake na makundi maalumu, kuwekeza katika masoko ya mitaji.
“Hatua hii imewezesha kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja kwa asilimia 520.41 na kufikia Sh. trilioni 4.4 Disemba 2025, ikilinganishwa na Sh. bilioni 701.46 Disemba 2021.
“Kuidhinishwa kwa Mfuko wa Ziada kunafanya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja hapa nchini kufikia 26, hivyo, tunatarajia mfuko huu kuchochea zaidi maendeleo na ustawi wa uchumi wanchi yetu. “
Kuhusu Mfuko wa Ziada amesema una malengo mahsusi ya kuwekeza katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika Hatifungani za Serikali, Hatifungani za Kampuni, Dhamana za Serikali za muda mfupi na Amana katika benki za biashara. 
Aidha, amesema Mfuko huo unatoa Bima ya Maisha (Life Insurance) kwa wawekezaji inayofikia asilimia 50 ya Thamani ya Uwekezaji, hivyo kuwafanya wawekezaji kufaidika na uwekezaji katika masoko ya mitaji; na kupata manufaa ya bima ya maisha.
“Bima ya maisha ni nguzo muhimu ya usalama wa kifedha kwa wananchi, kwani husaidia kulinda familia dhidi ya athari za kifedha zinazoweza kujitokeza endapo muwekezaji atafariki, kupata ulemavu wa kudumu, au kukumbwa na majanga yasiyotarajiwa.
“Kupitia bima ya maisha, familia huweza kuendelea na maisha kwa uthabiti, ikiwa ni pamoja na kuweza kugharamia mahitaji ya msingi kama elimu ya watoto, huduma za afya, na marejesho ya mikopo, hivyo kupunguza utegemezi wa kifedha kwa ndugu au jamii,”amesema CPA.Mkama
Akifafanua zaidi amesema Bima ya Maisha huchangia kukuza utamaduni wa kupanga na kujiandaa kwa siku zijazo, jambo linaloimarisha ustawi wa kaya na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Hivyo amesisitiza kuanzishwa kwa Mfuko wa Ziada ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 ambao pamoja na mambo mengine, una lengo la kuwezesha masoko ya mitaji kuwa na bidhaa bunifu zinazokidhi mahitaji ya wawekezaji, na hivyo kuchochea uchumi shindani, himilivu na jumuishi kwa maendeleo endelevu kwa watanzania wote.
Amesema ili kufikia malengo ya Mpango Mkuu wa Sekta ya Fedha, ni muhimu kwa wananchi kutumia fursa za uwekezaji zinazojitokeza, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Kuanzishwa kwa Mfuko wa Ziada ni mojawapo ya fursa za kufanikisha azma hii.
“Mfuko huu unatoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na kimataifa kushiriki na kuwezesha upatikanaji wa maendeleo endelevu kwa watanzania wote. Hivyo nawapongeza Bodi na Menejimenti ya Africa Pension Fund Limited kwa kuja na ubunifu huu.
“Pia Mfuko wa Ziada unaendeshwa na kampuni ya Africa Pension Fund Limited ambaye ni Meneja wa Mfuko na Benki ya NBC (NBC Bank Limited) ambaye ni Mtunza Dhamana wa Mfuko (Custodian).
“Aidha, Kampuni ya Alliance Life Insurance ndiyo kampuni inayotoa Bima ya Maisha (Life Insurance) kwa wawekezaji wa Mfuko huu. Nazipongeza sana Kampuni hizi kwa kuja na ubunifu wa kuanzisha Mfuko huu wenye manufaa makubwa kwa wananchi.”
Hata hivyo amesema uwekezaji katika Mfuko wa Ziada una manufaa katika ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi hapa nchini ikiwemo kuchangia katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuwezesha makundi mbalimbali ya jamii.
“Ikiwa ni pamoja na watu wa kipato cha chini kuwekeza kwa pamoja katika dhamana za masoko ya mitaji.Pia wawekezaji watapata faida ya ongezeko la thamani katika uwekezaji wao (Net Asset Value), ikiwa uwekezaji utafanyika kwa mujibu wa Sera ya Uwekezaji kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupata faida.
“Aidha mfuko huu unatoa anuwai ya uwekezaji kwa wananchi ambapo wawekezaji watapata fursa ya fedha zao kuwekezwa katika maeneo mbalimbali na hivyo kupunguza vihatarishi. “


