Madiwani Ilemela waagiza kodi ikusanywe bila kero

Mwanza. Baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela limepitisha mpango wa bajeti ya Sh101.74 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027, huku likitaka ukusanyaji wa mapato ufanyike kwa njia rafiki bila kuwasumbua au kutumia nguvu kwa walipa kodi.

Bajeti hiyo imepitishwa katika kikao maalumu cha baraza kilichofanyika leo Jumatatu, Januari 26, 2026, baada ya kupokea, kujadili na kuridhia mapendekezo yaliyowasilishwa na Mchumi wa Manispaa, Herbert Bilia.

Meya wa Manispaa ya Ilemela, Sarah Ng’whani, amesema baraza limeridhia bajeti hiyo baada ya kuzingatia vipaumbele vilivyopendekezwa, mahitaji ya wananchi na mwelekeo wa maendeleo ya halmashauri.

Mchumi wa Manispaa ya Ilemela, Herbert Bilia akiwasilisha mpango wa bajeti ya manispaa hiyo kwa mwaka 2026/27 katika baraza la madiwani.



Bajeti inalenga kuboresha utoaji wa huduma za jamii pamoja na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Amesisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mifumo rafiki, sambamba na utoaji wa elimu ya kodi ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi.

“Mnaokwenda kukusanya mapato, mkusanye kwa njia rafiki, msitumie nguvu. Tuwaelimishe wafanyabiashara maana mfanyabiashara akielewa, si mbishi kulipa kodi,” amesema Ng’whani.

Utoaji wa elimu ya kodi utasaidia kujenga uaminifu kati ya halmashauri na wananchi, hatua itakayoongeza mapato ya ndani na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mchumi wa Manispaa, Herbert Bilia, amesema bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 imezingatia vipaumbele vya kata zote 19 za manispaa, huku ikijikita katika kuboresha huduma za jamii na miundombinu.

Meya wa Manispaa ya Ilemela, Sarah Ng’whani akizungumza katika kikao maalumu cha kupitisha bajeti ya mwaka 2026/27 ya manispaa hiyo.



 Kaimu Mkurugenzi, Dk Maria Kapinga, amewataka watumishi na viongozi kushirikiana katika utekelezaji wa bajeti, hususan kwenye ukusanyaji wa mapato na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

Diwani wa Kata ya Nyakato, Jonathan Mkumba, na diwani wa Kata ya Kitangiri, Donald Ndaro, wamesisitiza ushirikiano kati ya madiwani, watumishi wa halmashauri na wananchi, huku wakihimiza uimarishaji wa vyanzo vya mapato na kukamilisha miradi viporo.

Diwani wa Viti Maalum, Sarah Manyama, alisema bajeti itasaidia kuboresha ustawi wa wananchi pamoja na miundombinu ya Manispaa ya Ilemela endapo itatekelezwa ipasavyo.