Dar es Salaam. Haijalishi ni kipindi cha mvua au kiangazi, kero ya majitaka kutoka kwenye chemba za baadhi ya mitaa ya Kariakoo jijini Dar es Salaam imeendelea kuwatesa wafanyabiashara, mamalishe na maelfu ya watu wanaofika eneo hilo kwa shughuli za kibiashara.
Katika mitaa kadhaa ikiwamo ya Uhuru, Msimbazi na Sikukuu, kumekuwa na majitaka yanayotiririka barabarani, hali inayosababisha harufu kali na mazingira machafu.
Licha ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kwa nyakati tofauti kuweka kambi Kariakoo ya kuikarabati miundombinu ya usafirishaji na utiririshaji majitaka ikilenga kuboresha usafi wa mazingira, changamoto hiyo bado ipo katika eneo hilo la kibiashara lenye watu wengi na msongamano mkubwa.
Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi kwa nyakati tofauti Januari mwaka huu, umebaini ujenzi unaoendelea Kariakoo ni miongoni mwa sababu za uwepo wa hali hiyo.
Majitaka yakiwa yanatoka kwenye chemba katika mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam.
Mbali ya hayo, utupaji wa taka ngumu katika mifumo ya majitaka kama vile nguo, mawe, matairi na plastiki unatajwa kuchangia hali hiyo.
Akizungumza na Mwananchi, mfanyabiashara anayepanga bidhaa Mtaa wa Sikukuu na Mchikichi, Salehe Othman anasema tatizo hilo limekuwa likiwaathiri moja kwa moja kwa kuwa wateja hushindwa kusimama au kukagua bidhaa.
“Majitaka yakitoka, eneo lote linanuka. Mteja hawezi kusimama hapa, anapita kwa haraka au anakwenda sehemu nyingine,” anasema.
Shaaban Salum, mfanyabiashara wa vyombo eneo hilo, anasema hali huwa mbaya zaidi mvua kubwa inaponyesha, Kariakoo hugeuka bwawa na kwa baadhi ya maeneo kinyesi huelea.
“Unapanga mzigo hujatulia vizuri unaona maji yanaanza kutoka kidogokidogo mwisho wa siku yanatiririka yakiambatana na kinyesi. Ikinyesha mvua hali inakuwa mbaya zaidi,” anasema.
Mamalishe katika Mtaa wa Uhuru na Sikukuu, Zainabu Zawadi anasema tatizo hilo ni kikwazo kwa shughuli zao za kila siku, kwa kuwa hujikuta katika wakati mgumu pale baadhi ya chemba zinapofumuka na kutiririsha majitaka.
“Watu wakiona majitaka yanapita karibu na nilipoweka vyakula ni ngumu kununua maana wanawaza maji yanayotiririka yanayotokea kwenye ghorofa za jirani,” anasema.
Majitaka yakiwa yametwama katika mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam ambayo imekuwa kero kwa wafanyabiashara na wananchi wanaofika katika eneo hilo.
Wapitanjia wanaeleza kuchoshwa na hali hiyo, wakisema kuna wakati hulazimika kupita katikati ya majitaka au kubadilisha njia hali inayoongeza usumbufu na hatari za kiafya.
Sauda Shaibu, anasema wavaaji wa nguo ndefu huteseka wakilazimika kuzishikilia vinginevyo huburuza kwenye majitaka.
“Wavaa magauni marefu tuna wakati mgumu, unajikuta unakumbatia gauni ili kuepuka maji machafu. Kwa mfano, ukipita Barabara ya Msimbazi, pikipiki na magari hupita hivyo unaogopa kurushiwa maji machafu,” anasema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary anasema majitaka katika eneo hilo ni tatizo sugu kutokana na ujenzi unaoendelea unaoziba baadhi ya mifumo na mitaro ya maji.
“Tuliambiwa mifumo yote ya zamani itatolewa na kuwekwa mipya, tunasubiri. Kingine kinachochangia hali hii ni ujenzi unaoendelea kwa kuziba mifumo iliyokuwapo, hivyo maji yakifika eneo lililozibwa hakuna njia, lazima yatoke nje,” anasema.
Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam, Issack Mtega, anasema hali ya majitaka kutiririka eneo la Kariakoo inasababishwa kwa kiasi kikubwa na uunganishaji holela wa mifumo ya majitaka kwenye maji ya mvua.
Majitaka yakiwa yanatiririka katika mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam ambayo imekuwa kero kwa wafanyabiashara na wananchi wanaofika katika eneo hilo.
Mtega anasema mfumo wa maji ya mvua ulijengwa mahususi kwa ajili ya kupitisha maji hayo pekee, lakini kwa sasa umeingiliwa na mifumo ya majitaka, jambo linaloharibu ufanisi wake.
“Watu wameunganisha majitaka kwenye mifumo ya maji ya mvua. Matokeo yake ikinyesha au watu kumwaga maji kwenye vyoo vyao yanarudi juu na kujaa mitaani yakiwa machafu,” anasema.
Anaeleza kutokana na hali hiyo, mkakati uliopo ni kupita nyumba kwa nyumba kukagua mifumo ya majitaka na endapo itakuwa imeelekezwa sehemu tofauti muhusika atatakiwa kuondoa kuelekeza inapotakiwa.
“Tatizo hili liko Kariakoo nzima na mjini kuna baadhi ya maeneo tunahitaji kufanya tathmini upya, hata kufikia hatua ya kutumia wataalamu washauri ili kuangalia mfumo mzima kwani tumekuwa tukitenga bajeti ya uzibuaji hadi Sh300 milioni kwa mwaka,” anasema.
Anasema kwa sasa Kariakoo kuwe na mvua au jua hali zinafanana kwa sababu watu wamebadilisha mifumo, hivyo wakazi na wafanyabiashara hutembea ndani ya maji machafu.
“Unakuta watu wanatembea kwenye maji yanayochanganyika na majitaka hii ni hatari kubwa kwa afya na mazingira,” anasema.
Mtega anakiri ujenzi unaoendelea Kariakoo umechangia kuzorota kwa mifumo ya awali ya majitaka na maji ya mvua, akieleza baadhi ya mifereji imezibwa au kujengwa juu yake bila kuzingatia ramani za miundombinu.
“Zamani kulikuwa na mifumo ya majitaka na storm water (maji ya mvua), lakini mingi imezibwa. Watu wanajenga bila kuzingatia mifumo iliyopo chini ya ardhi,” anasema.
Majitaka yakiwa yametwama katika mitaa ya Kariakoo, Dar es Salaam ambayo imekuwa kero kwa wafanyabiashara na wananchi wanaofika katika eneo hilo.
Anaeleza baadhi ya maeneo, Serikali iliboresha kwa kuweka mifumo mipya, lakini bado kuna ya zamani ambayo haikubadilishwa hali inayosababisha maji kushindwa kupita vizuri.
Mkurugenzi wa Idara ya Majitaka wa Dawasa, Lidya Ndibalema anasema uzibaji hutokea mara kwa mara kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya mifumo ya majitaka, ikiwamo utupaji wa taka ngumu kwenye vyoo na mitaro.
Anasema Dawasa imeweka timu maalumu zinazofanya kazi saa 24 ili kukabiliana na uzibaji unapotokea, iwe ni mchana au usiku.
Anaeleza magari ya kunyonya majitaka na mashine za kisasa za kusafisha laini kwa msukumo wa maji hutumika kufanya kazi hiyo.
“Uzibaji ni wa kawaida kwa sababu watu wanatumia vyoo kila siku, kuna vitu vinakwama kwenye laini na kuziba. Tunapofanya shughuli hiyo mara nyingi tunakuta michanga. Tukipata taarifa, timu zetu zinaingia kazini mara moja,” anasema.
Ndibalema anasema usafishaji wa mifumo ya majitaka haufanywi tu wakati wa dharura, bali ni kazi endelevu ya matengenezo ya kawaida, ambayo laini husafishwa kwa vipande vipande ili kuzuia uzibaji mkubwa.
Anasema Dawasa pia inaendelea na ujenzi wa mitambo ya kisasa ya majitaka katika maeneo mbalimbali, yakiwamo ya Buguruni na Jangwani.
Anaeleza mabomba makubwa yanatoka maeneo ya uzalishaji wa majitaka, yakipitia katikati ya jiji kama Upanga, kisha kufika vituo vya kukusanya na kupampu majitaka kwenda kwenye mtambo mkuu wa matibabu.
“Mtambo huu mkubwa unaambatana na ukarabati wa mifumo ya zamani iliyochakaa ili kuongeza uwezo wa kukusanya na kutibu majitaka yanayozalishwa na ongezeko la watu jijini,” anasema.
Ndibalema anasema mafanikio ya kudhibiti uzibaji yanategemea ushirikiano wa wananchi kwa kutumia mifumo ya majitaka kwa usahihi na kutoa taarifa mapema pindi tatizo linapojitokeza.
“Changamoto inaweza kujirudia. Leo tumesafisha, kesho ikaziba, ndiyo maana tuna timu zetu ziko ‘standby’ muda wote. Lakini wananchi wakitumia mifumo vizuri, tatizo litapungua,” anasema.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Januari 14, 2026 alisema ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Korea utaimarisha huduma ya majitaka kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.
Aweso aliyefanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania, Ahn Eunju, alisema Serikali za Tanzania na Korea zinashirikiana kutekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya usafi wa mazingira jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Dola 90 milioni za Marekani (Sh223.65 bilioni) unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi wanaokadiriwa kufikia milioni 1.8 katika jiji hilo unaotekelezwa na Dawasa.
Katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma, yalijikita katika masuala mbalimbali ya ushirikiano, hususani maeneo ya kuimarisha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, rasilimali za maji na usalama wa maji, majitaka, uvunaji wa maji ya mvua na fursa za uwekezaji katika sekta ya maji.
Aweso alisema halmashauri za Jiji la Dar es Salaam na Kinondoni ndiyo maeneo mradi huo unatekelezwa na mpaka sasa umefikia asilimia 10.8.
Alisema mradi utasaidia kuboresha mfumo wa majitaka yanayozalishwa baada ya matumizi ya majisafi yanayotarajiwa kuongezeka.
Alisema mtambo wa kisasa wa kuchakata majitaka eneo la Buguruni utawezesha kuachana mfumo wa zamani wa kuchakata majitaka kwa kutumia mabwawa unaotumika hivi sasa.