Dar es Salaam. Katika juhudi za kuwasaidia wawekezaji kuweka akiba na kukuza fedha zao kupitia uwekezaji wenye nidhamu katika soko la fedha, Africa Pension Fund Limited (APeF) imezindua rasmi mfuko wa ziada, ambao ni wa kwanza wa uwekezaji wa pamoja katika soko la fedha nchini Tanzania unaojumuisha mafao ya bima ya maisha.
Mfuko huo umezinduliwa leo Januari 26, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo kipindi cha awali cha uuzaji wa vipande vya uwekezaji kinaanza leo na kinatarajiwa kumalizika Februari 25, 2026. Hatua hiyo inaweka alama muhimu katika kupanua upatikanaji wa suluhisho za uwekezaji zilizo chini ya udhibiti wa mamlaka husika.
Mbali na kutoa fursa ya kukuza mtaji, mfuko huo una faida ya ziada ya ulinzi wa bima ya maisha kwa wawekezaji binafsi wanaokidhi vigezo. Pia umeundwa kwa urahisi wa matumizi, ukiwawezesha wawekezaji kuanza kwa kiwango kidogo, kuongeza uwekezaji wakati wowote na kupata fedha zao ndani ya siku tatu za kazi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa APeF, Mfaume Kimario, amesema mfuko wa Ziada umeundwa kwa wawekezaji wanaotaka njia rahisi, salama na za kuaminika za kukuza fedha zao bila kupoteza uwezo wa kuzifikia pindi zinapohitajika.
“Huu ni mfuko imara katika soko la fedha unaopatikana kwa urahisi, wenye ulinzi wa bima ya maisha kwa wawekezaji wanaokidhi vigezo, ukianzia na thamani halisi ya uwekezaji ya chini kabisa ya Sh250,000,” amesema Kimario.
Ameeleza kuwa bima hiyo hutoa kinga sawa na asilimia 50 ya thamani halisi ya uwekezaji hadi kiwango cha juu cha thamani kilichohakikishwa cha Sh100 milioni, huku kiwango cha juu cha malipo ya bima kikiwa Sh50 milioni.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti na Bodi ya Wakurugenzi, Mjumbe wa Bodi ya APeF, Dk Hamisi Kibola, ameipongeza Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa hatua zilizofikiwa katika kukuza na kuimarisha masoko ya mitaji nchini.
Amebainisha kuwa kiwango cha uwekaji akiba nchini bado kipo chini ya asilimia 3, na kutoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya wasimamizi na wadau wa sekta ya fedha ili kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba unaozingatia taaluma, uaminifu, elimu ya fedha na upatikanaji wa huduma.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama, amesema kuidhinishwa kwa mfuko wa ziada kumeongeza idadi ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja nchini kufikia 26, hatua inayochochea zaidi maendeleo ya sekta ya uwekezaji Tanzania.
