SAA chache tangu mshambuliaji George Mpole kusaini mkataba wa miezi sita kuitumikia Tanzania Prisons, amesema anafurahia kurejea kazini baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, tangu alipoachana na Pamba Jiji katika usajili wa dirisha lililopita, huku akiweka hadharani malengo aliyonayo kwa maafande hao.
Wakati Mpole anaachana na Pamba alikuwa ameifungia mabao mawili, kitu anachokitamani katika mechi zilizosalia kwa msimu huu ni kutajwa katika orodha ya wafungaji wa mabao mengi, japo anajua atakuwa na kibarua kigumu kutokana na ugumu wa Ligi ya msimu huu.
“Nafasi yangu ni kufunga kwa mechi zilizochezwa mchezaji aliye na mabao mengi ni matano, bado nina nafasi ya kupambana kuhakikisha na mimi nafunga mabao kwa ajili ya kuisaidia timu,” amesema Mpole aliyekuwa mfungaji bora wa mabao 17 msimu wa 2021/22 akiwa na Geita Gold.
Mpole amesema mkataba wa miezi sita aliyosaini na Prisons,utatoa taswira kwa kiwango atakachoonyesha endapo kama viongozi watamuongezea mwingine au la.
“Sio muda wa kuzungumza sana, kwani ndio kwanza nimejiunga na timu, nahitaji muda wa kupambana zaidi kuhakikisha tunakuwa katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu Bara,” amesema Mpole aliyewahi kuitumikia pia Real Nakonde ya Zambia, Mbeya City na FC Lupopo ya DR Congo.
Kabla ya mechi ya jana Jumapili Prisons ilikuwa imeshinda mbili, sare moja, imefungwa tano, mabao ya kufunga matatu ya kufungwa sita,ilikuwa na pointi saba.
Mwanaspoti lilipata taarifa nyingine kutoka chanzo cha ndani cha timu hiyo, kumalizana na kiungo Gustavo Saimon aliyetokea Coastal Union ya Tanga, japo taarifa zingine zinasema ametua Dodoma Jiji.
