Msiba wa Mtei ulivyoibua mijadala ya kisiasa

Dar es Salaam. Fursa ya kutema nyongo, ndio tafsiri iliyotolewa na wachambuzi wa siasa kuhusu kauli za wanasiasa wa vyama vya upinzani walizozitoa katika jukwaa la maombolezo ya msiba wa mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, kilichozungumzwa na wanasiasa kwenye safari hiyo ya mwisho wa Mtei, aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kinaashiria kuwepo ombwe la jukwaa huru la wao kuzungumza na wakasikilizwa, hivyo msiba wameutumia kutema nyongo.

Wanasiasa hao, walitema nyongo hizo mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan juzi Jumamosi, Janauri 24, 2026 kwenye maziko ya Mzee Mtei (93) yaliyofanyika nyumbani kwake, Tengeru, mkoani Arusha.

Mzee Mtei aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha katika utawala wa awamu ya kwanza wa hayati Mwalimu Julius Nyerere alifariki dunia usiku wa Januari 19, 2026 nyumbani kwake Tengeru.

Katika safari yake ya mwisho hapa duniani, mamia ya waombolezaji walijitokeza wakiwamo wanasiasa na kupata fursa ya kutoa salamu zao ikiwamo kuchambua mchango wa Mzee Mtei na kuonesha dosari la kiutawala na demokrasia.

Wakati viongozi wa upinzani wakionesha matobo hayo, waombolezaji waliokuwapo walikuwa wakishangilia huku Dk Mwigulu akionekana mara kadhaa kutikisa kichwa na kwenye mazungumzo yake alisema ameyapokea na wanakwenda kuyafanyia kazi.


Miongoni mwa waliozungumza na kuibua shangwe ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alionesha dosari katika demokrasia nchini, inayofanya Taifa kuwa na maumivu.

Mbowe amesema baadhi viongozi wa upinzani wapo magerezani kwa kile alichokiita kesi za kubumba.

“Waziri Mkuu utambue wewe na viongozi wa Serikali kwamba Taifa letu bado lina maumivu makubwa sana, nitakuwa mnafiki au Mswahili nisipolisema hili. Maendeleo ambayo umetueleza kwamba Serikali itasimamia ni jambo jema, tutashukuru lakini hakuna jambo la maana na muhimu kuliko uhuru wa watu katika nchi yao.

“Njia bora kuliko zote za kuleta maendeleo katika nchi, rejesheni kwanza uhuru na mkiri ukweli pale ambako Serikali ilipokosea isione kusema ilikosea hapa turekebishe,” amesema Mbowe.

Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho aliyepo gerezani kwa kesi ya uhaini, Tundu Lissu ameandika hotuba iliyowasilishwa msibani hapo, akiambatanisha salamu zake za rambirambi na kumsifu Mtei kwa ujasiri, huku akipinga uchawa.

“Kwa ujasiri huohuo, aliwajibika kwa kujiuzulu nafasi pale Mwalimu Nyerere alipomkatalia ushauri wake huo. Alikuwa na uadilifu wa kuona haikuwa sahihi kwake kuendelea kutumikia nchi wakati ametofautiana na kiongozi mkuu wa Serikali.

“Leo hii, kwa jinsi ambavyo ‘uchawa’ umekuwa ni donda ndugu na umekithiri ngazi zote za utumishi wa umma na hata katika sekta binafsi, tunaweza kupima kiwango cha juu cha ujasiri wa Mzee Mtei na uzalendo wake kwa nchi yetu,” ameandika Lissu.

Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameuelezea ujasiri wa Mtei alipoandika barua ya kujiuzulu kwa Mwalimu Nyerere, huku akidokeza tofauti za kisiasa hazikuzaa utekaji na mauaji ya raia.


“Wazee wenzetu walitofautiana bila kuchukiana, walikuwa na misimamo tofauti bila kugombana, walikuwa na mawazo tofauti bila kutekana, waliamua tofauti bila kuuana.

“Heshima ya mtu, kutotweza utu wa mtu ilikuwa tunu kubwa kwao. Ni wajibu wetu kutafakari na kupata njia yetu ya kutofautiana bila kuvunjiana heshima, bila kupigana, bila kuuana, bila kutekana,” amesema Zitto.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche ameeleza msimamo unaoonekana katika chama hicho sasa, msingi wake ni aliyekiasisi Mzee Mtei.

“Kwa wale mnaotuona sisi Chadema na misimamo yetu ni kwa sababu ya DNA (vinasaba) ya mwasisi wetu. DNA sio kuficha jambo lifanyike la ovyo. Mtei aliacha uwaziri kwa sababu ametofautiana na Rais. Lakini sasa hivi ingekuwa hatari kwa sababu angepotea au lolote lingempata,” amesema Heche.


Kwa jumla, kila mwanasiasa wa upinzani aliyepata nafasi ya kuzungumza, aliomboleza kwa kuambatanisha na changamoto za haki, demokrasia, uhuru wa kuongea na kuonesha dosari katika demokrasia kama inavyoelezwa na Mwandishi wa Vitabu, Maundu Mwingizi.

Mwingizi anaona kila kiongozi wa chama cha upinzani aliyesimama kuzungumza, muktadha wa ujumbe wake ulikuwa kutoweka kwa uhuru wa wananchi na kuminywa kwa demokrasia.

“Ukimsikiliza hata Mbowe (Freeman) ambaye hakutarajiwa, lakini alilalamikia kuwepo kwa viongozi wa upinzani magerezani, Zitto Kabwe ameonesha uamuzi wa Mtei kwa Nyerere kujiuzulu pengine ingekuwa sasa angepotea,” amesema.

Ameeleza viongozi karibu wote wa upinzani waliozungumza, walionesha changamoto za utawala, walidai haki na uhuru wa wananchi.

Mwingizi amesema wazungumzaji wanaonesha kuwepo kwa tatizo katika demokrasia ya nchi na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu hakulipinga hilo, zaidi ya kukubali kwamba atayabeba na kuyafanyia kazi.

Hata hivyo,  amesema suala sio kuyabeba na kuyafanyia kazi pekee, bali ni kuhakikisha watu wanapata haki kwanza ndio kuanza hatua hizo tarajiwa.

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa, Dk Rehema Kilinda amesema kilichotokea kinaashiria, kuna uhaba wa majukwaa huru ya kuwakutanisha viongozi wa Serikali na vyama vya upinzani kuzungumza mambo yaliyozungumzwa.

“Wakati uhuru wa kisiasa ukiminywa, wanasiasa hutafuta majukwaa mbadala. Msiba, harusi au ibada za kidini hugeuka majukwaa ya kisiasa kwa sababu ni vigumu kuyadhibiti,” amesema Dk Kilinda.

Amesema si kwamba viongozi wa upinzani wanapenda kuchanganya msiba na siasa, bali wanalazimishwa na mazingira.

Mtazamo unaokaribiana na huo, umetolewa pia na mtaalamu wa siasa na utawala Dk Abdallah Nchimbi kuwa, kilichotokea kinaashiria kuna ombwe la fursa za uhuru wa kuueleza ukweli.

“Msiba uliwakutanisha Serikali, chama tawala na upinzani bila itifaki. Wakati majukwaa rasmi ya mazungumzo hayapo au hayafanyi kazi, msiba unageuka eneo la mazungumzo ya kitaifa yasiyo rasmi,” amesema.

 “Ukipuuza Bunge, vyombo vya maridhiano na mikutano ya hadhara, ujumbe hautapotea utatafuta njia nyingine. Msiba ni moja ya njia hizo,” amesema DK Nchimbi.

Amesisitiza kitendo cha kuzungumza mbele ya Serikali kwenye msiba kinaashiria upinzani hauoni tena tofauti kati ya majukwaa rasmi na yasiyo rasmi.

Dk Nchimbi amesema hotuba za kisiasa kwenye msiba wa Mtei ni kielelezo cha mkwamo wa kisiasa nchini na inaashiria kukosekana kwa majukwaa huru ya mazungumzo.

“Pia, inaashiria kuna mwendelezo wa mvutano kati ya Serikali na upinzani, na hamu ya pande zote kusikilizwa nje ya mifumo rasmi,” amesema.

Mtaalamu wa Historia ya Siasa, Dk Jonas Luhanga amesema hotuba hizo ni sehemu ya mkakati wa kisiasa wa kuzungumza moja kwa moja na wafuasi.

“Hakuna kampeni, hakuna itifaki kali. Kuna wananchi, wanahabari na Serikali. Ujumbe unaotolewa hapo unakwenda mbali zaidi kwa sababu unatolewa katika mazingira ya uhalisia na hisia kali,” amesema Dk Luhanga.

Amesema kwa upande wa Chadema msiba wa Mtei ulikuwa pia nafasi ya kuonesha bado wanaungwa mkono na wana sauti, ndio maana walionekana kutumia jukwaa hilo kuzungumza siasa.

Dk Luhanga amesema kilichotokea katika msiba huo si bahati mbaya, bali ni kielelezo cha joto la siasa nchini.

Amesema wa Mtei umeonesha jinsi majonzi binafsi yanavyogeuka kuwa majukwaa ya mijadala ya kitaifa, inayoendelea kwa wakati husika.

“Pale ambapo siasa zinakosa pumzi, nyakati kama za misiba inayokutanisha makundi yote, zinatumika kutema nyongo,” amesema Dk Luhanga.

Maneno ya Mbowe sahihi, lakini…

Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo amejikita kwenye hoja za Mbowe, akisema amezungumza wakati ambao mwaka na zaidi umepita chama chake kikipitia dhoruba lukuki bila yeye mwasisi kusema.


“Kwanini usubiri msiba ndio uutumie kuzungumza na mbona aliwahi kuonekana kwenye matukio mbalimbali akahojiwa hakusema. Ujumbe mzuri umewasilisha haja za msingi, lakini umechelewa sana,” amesema Dk Masabo.

Amesema ingawa alichozungumza ni muhimu na kitasaidia, bado watu hawawezi kumwamini, kwa sababu amechelewa kusema alichokisema, tayari watu walishaumizwa.

 “Ujumbe ule watu wanaupokea lakini watu hawamuamini Mbowe. Mtawala unakuwa umemgonga kwa hoja, lakini kwa hadhira yako unakuwa hujafanya kitu kikubwa,” amesema.