YANGA imerejea nchini jana Jumapili ikitokea Misri ilipoenda kucheza mechi ya tatu la Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Al Ahly itakayorudiana nao wikiendi, lakini kuna hesabu mpya zinapigwa na kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves dhidi ya Waarabu hao kabla ya pambano hilo.
Hilo lilikuwa pambano la kwanza kwa Yanga kupoteza hatua ya makundi, ila ni kipigo cha pili msimu huu katika michuano hiyo, kwani awali ili[poteza 1-0 mbele ya Silver Strikers ya Malawi katika raundi ya pili na sasa itakuwa na kazi ya kushinda mechi hiyo ya marudiano na nyingine mbili za Kundi B ili iende robo fainali.
Timu hizo zitarudiana Jumamosi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja unaotumiwa na Yanga kama uwanja wa nyumbani sambamba na Singida Black Stars na Azam FC zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika ambapo jana zilikuwa uwanjani kukamilisha mechi za raundi ya tatu ya makundi yao ya B na C mtawalia.
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kuwasili, Pedro aliyepoteza pambano la kwanza tangu ajiunge na Yanga, amesema licha ya timu hiyo kupoteza mechi hiyo ya kwanza katika hatua hiyo, bado anaona Yanga ina nafasi kubwa ya kulipa kisasi na kujiweka pazuri kwenda robo fainali na mikakati ameshaianza mapema.
Pedro amesema mikakati yao inaenda sambamba na ya mechi ya kiporo cha Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji inayopigwa kesho kwenye Uwanja wa KMC kabla ya timu kwenda Zanzibar kuisubiri Al Ahly yenye pointi sana kwa sasa na kuongoza Kundi B lenye As FAR Rabat ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria.
Kocha huyo raia wa Ureno amesema, mara baada ya mechi ya Ligi dhidi ya Dodoma Jiji haraka watatua Zanzibar tayari kwa mchezo wa kulipa kisasi.
Kocha huyo amesema wachezaji wake waliumia na matokeo ya mechi hiyo ya ugenini dhidi ya Ahly na makocha pia wameshajua makosa yaliyosababisha wapoteze wikiendi iliyopita na kwamba watarekebisha hasa baada ya kujua pia upungufu wa wapinzani wao hao na kuwatengenezea mikakati ya kuwamaliza nyumbani.
“Tumepoteza mchezo mmoja, haiwezi kuwa sababu ya kutuondolea utulivu na wala kuharibu malengo yetu, sisi sio timu ya kukata tamaa, jambo zuri wachezaji wangu wamejua wapi walikosea na sisi makocha tunajua wapi kwa kurekebisha,” amesema Pedro aliyeongeza;
“Leo (jana) tutapumzika kidogo, tutarudi katika mazoezi kwa ajili ya mchezo wa ligi na tukimaliza hapo tutaanza kuangalia hii mechi ya marudiano, tutakapokuwa nyumbani.
“Tuna nafasi ya kufuzu kwemnda hatua inayofuata lakini tunatakiwa kubadilisha matokeo yetu, tunajua kipi kifanyike ili tuweze kushinda, hilo lipo kwenye uwezo wetu.”
Yanga itakutana na Dodoma Jiji kesho Jumanne ikiwa na kumbukumbu ya kushinda kwa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa katika mechi iliyopita kabla ya Yanga kwend Cairo kuvaana na Al Ahly na kupoteza 1-0.
Mechi ijayo ya CAF dhidi ya Ahly, timu hizo zitakuwa zimeanza duru la pili la hatua ya makundi, kwa sasa kila moja kundini imeshacheza mechi tatu, huku Yanga ikiwa ya pili na alama nne ikifuatiwa na as FAR Rabat na JS Kabylie ambazo kila moja ina pointi mbili, huku zikirudiana pia wikiendi huu.
Pia Pedro aliongeza ana imani na wachezaji wake watabadilika na kucheza kwa ushindi wakiwa nyumbani ili kuongeza nafasi ya uwezekano wa kufuzu.
“Nina imani sana na wachezaji wangu, wana ubora wa kuweza kusahihisha makosa yao kwenye mchezo ujao, tutafanya mabadiliko machache kwenye mchezo wa ligi ili kutunza ubora wa wachezaji.”
Msimu uliopita Yanga ikwama kutinga robo fainali baada ya kumaliza mechi sita ikivuna pointi nane tu, ikizidiwa na Al Hilal ya Sudan iliyoongoza kundi na MC Alger zilizofuzu hatua hiyo, japo nazo zikiishia njiani.