Dar es Salaam. Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara amemteua mdogo wake, Tene Ouattara kushika wadhifa mpya ulioundwa wa naibu waziri mkuu.
Hatua hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti nchini humo, ikitafsiriwa kama sehemu ya mabadiliko makubwa ya kisiasa ndani ya serikali yake.
Uteuzi huo uliofanyika Ijumaa ya Januari 23, 2026 ni mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyopewa jina la Mambe II, yaliyofanyika siku mbili tu baada ya Robert Mambe kuthibitishwa tena kuwa waziri mkuu kufuatia ushindi wa chama tawala katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika Desemba 2025.
TeneĀ Ouattara anayejulikana kwa jina la utani Photocopy kutokana na kufanana kwake kwa karibu na Rais atahudumu katika wadhifa huo mpya wa juu, huku akiendelea kubaki pia kama waziri wa ulinzi nafasi yenye ushawishi mkubwa ndani ya serikali na vyombo vya usalama vya taifa.
Mabadiliko hayo ya kimuundo yanamweka Ouattara mdogo katika kilele cha ngazi za utawala hatua ambayo wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema inalenga kuimarisha udhibiti wa Rais mwenye umri wa miaka 84, anapoanza muhula wake wa nne madarakani.
Kwa ujumla baraza la mawaziri lenye mawaziri 35 limeonesha mwendelezo wa uongozi badala ya mabadiliko makubwa.
Viongozi wakuu wakiwemo Makamu wa Rais, Tiemoko Kone na Waziri wa Mambo ya Ndani, Vagondo Diomande wameendelea kubaki katika nyadhifa zao ishara ya serikali kuendeleza utawala uliokuwepo awali.
Hatua hiyo pia inatajwa kuwa inaakisi mkakati wa kuhakikisha uthabiti wa kiutawala wakati Ivory Coast ikiendelea kushuhudia ukuaji wa uchumi na kuvutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Hata hivyo, kuanzishwa kwa wadhifa wa TeneĀ kumeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi kuhusu mustakabali wa uongozi wa taifa hilo.
Wachambuzi wengi wa siasa nchini humo, wanatafsiri hatua hiyo kama mkakati wa kumwandaa mrithi wa kuaminika wa Rais na kuimarisha mamlaka ndani ya familia ya Ouattara.
Kwa mujibu wa vyama vya upinzani uteuzi huo unaashiria kurejea kwa siasa za mtu mmoja na kupunguza ushindani wa haki katika uongozi wa taifa.
Hata hivyo, chama tawala cha Rally of Houphouetists for Democracy and Peace (RHDP) kimetetea uamuzi huo kikisema ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa taifa na kuongeza ufanisi wa kiutawala katika moja ya uchumi imara zaidi Afrika Magharibi.
