Matumizi ya mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, X, WhatsApp na TikTok yanazidi kubadilika, huku baadhi ya watumiaji wakiigeuza kuwa majukwaa ya kutafuta suluhisho la changamoto za kifamilia na mahusiano.
Masuala ya malezi, ukatili wa kijinsia, manyanyaso ndani ya ndoa na maumivu ya kimapenzi ni miongoni mwa matatizo yanayowafanya watu kuwafuata watu maarufu mitandaoni kuomba ushauri, badala ya kutumia mabaraza au wataalamu waliopo katika mifumo rasmi.
Kwa upande wake, Serikali kupitia wataalamu wa saikolojia, maofisa ustawi wa jamii kuanzia ngazi ya vijiji pamoja na mabaraza ya usuluhishi imekuwa ikitoa huduma za ushauri na utatuzi wa migogoro ya kifamilia, ukatili wa kijinsia na changamoto za kijamii. Hata hivyo, ongezeko la idadi ya watu na matatizo ya kijamii limezidi uwezo wa wataalamu waliopo.
Pamoja na hilo, wapo wataalamu wa saikolojia waliotambulika na Serikali ambao wameanzisha madawati ya ushauri nasaha katika ofisi binafsi wakisaidia jamii. Lakini, baadhi ya watu wameamua kutumia mitandao ya kijamii kueleza changamoto zao na kuomba ushauri wa wazi kwa jamii nzima.
Mwandishi wa vitabu, Hanifa Kafashe, anayefahamika kupitia huduma ya ‘Malkia wa Kiha’, anasema idadi ya watu wanaomtafuta kuomba ushauri kupitia mitandao imekuwa ikiongezeka kila siku. Anasema hupokea visa kati ya 20 hadi 30 kwa siku kupitia Messenger ya Facebook.
“Watu wanakuamini kwa sababu wanajua matatizo wanayopitia si mapya. Tatizo langu linampata na mwingine, na likiwekwa wazi wengi wanajifunza na kupona kwa pamoja. Ni maumivu ya nafsi, mtu anaona ni rahisi kuzungumza na asiyemfahamu,” anasema Hanifa.
Anataja sababu mojawapo kuwa ni urahisi wa kupata msaada kwa haraka kupitia mitandao inayotumiwa na watu wengi. Pia, watu huona ni rahisi kuwafikia wanaowafuatilia na kuamini kuwa wamekuwa wakigusa maisha yao kupitia maudhui wanayoyasoma au kuyatazama.
Sababu nyingine ni uhuru wa kueleza changamoto bila kufahamika, hasa zinapokuwa nzito au za aibu. Hali hiyo huwafanya watu kuiona mitandao kama eneo salama la ‘kutema nyongo’.
Mtaalamu wa saikolojia, Milton Tunge, anasema wengi hushindwa kueleza changamoto zao kwenye mabaraza ya kata kwa kuhofia kufahamika na jamii inayowazunguka.
“Mabaraza mengi yanahusisha watu unaowafahamu, hivyo mtu anaogopa kuvuliwa heshima au siri zake kujulikana,” anasema.
Baadhi ya wananchi pia wanaamini gharama za kupata ushauri katika ofisi binafsi ni kubwa, hivyo mitandao huonekana kuwa njia mbadala isiyo na gharama. Aidha, shinikizo la umma mitandaoni huonekana kuwa na nguvu katika kushinikiza uwajibikaji, hasa kwenye matukio ya ukatili wa kifamilia.
Vilevile, baadhi ya watu hukwepa mifumo rasmi wakiamini kuna urasimu na ucheleweshaji wa maamuzi katika mabaraza ya usuluhishi, hali inayochelewesha utatuzi wa changamoto zinazohitaji majibu ya haraka.
“Huku baraza la kata linaweza kukupa ratiba ya kusikilizwa baada ya siku kadhaa, wakati changamoto yako inahitaji suluhisho la haraka,” anasema Tunge.
Anaongeza kuwa ongezeko la maarifa kutokana na maendeleo ya teknolojia limeifanya jamii kuamini kuwa mitandao ina wataalamu wa fani mbalimbali wanaotoa mitazamo tofauti ikilinganishwa na mabaraza yanayotumia zaidi uzoefu.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Geita, Frank Moshi, anakiri kuwa licha ya Serikali kuweka mifumo rasmi ya usuluhishi kuanzia ngazi ya mitaa hadi juu, baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia mitandao kama njia ya kushinikiza suluhisho la haraka.
“Baadhi ya wananchi wameanza kupoteza imani na mifumo rasmi ya utatuzi wa changamoto, ama kwa kujua au kutokujua,” anasema Moshi.
Pamoja na fursa zilizopo, mtaalamu wa saikolojia na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Robert Rwiza, anaonya kuwa mitandao ya kijamii bado haina uhakika wa kutosha katika kulinda faragha za watu. Anasema taarifa zinaweza kutumiwa vibaya au kuhaririwa.
“Japo jina halitajwi, watu wa eneo husika wanaweza kumtambua muhusika, jambo linaloweza kumuumiza zaidi,” anasema Rwiza.
Anaongeza kuwa ushauri wa ana kwa ana una faida zaidi kwa kuwa mtaalamu huweza kutambua hali ya kihisia kupitia mwonekano wa mshauriwa, jambo linalosaidia kutoa ushauri sahihi zaidi.
Moshi naye anakubaliana na hilo, akisisitiza kuwa licha ya changamoto za mifumo rasmi, ushauri wa ana kwa ana una mchango mkubwa katika kupata suluhisho la kudumu, ikilinganishwa na shinikizo la mitandao ya kijamii.