Arusha. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanza mchakato wa maombi ya kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya baada ya kukamilisha ujenzi wa jengo jipya lenye ghorofa tano litakalopunguza msongamano wa wagonjwa.
Hatua hiyo imetokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa alioukuta leo Jumatatu, Januari 26, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa kituo hicho kilichopo katikati ya jiji na kutatua changamoto zinazokikabili.
“Huu msongamano ni mkubwa, nataka mgonjwa akija ahudumiwe kwa wakati kisha aendelee na majukumu ya kiuchumi, lakini ninavyoona hapa haiwezekani, leteni maombi ya kujenga vituo vipya kwa sababu Serikali ina fedha na haitaki watu wakae muda mrefu kwenye foleni kusubiri huduma za afya,” amesema Mchengerwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, John Kayombo amesema baada ya kituo hicho kuweka vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Sh1.2 bilioni, idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kiuchunguzi imeongezeka na jiji lipo katika hatua za mwisho za kukamilisha ununuzi na ujenzi wa jengo la ghorofa tano.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza na wagonjwa waliokua wakisubiri huduma katika Kituo cha Afya Kaloleni jijini Arusha leo, Januari 26,2026. Picha na Filbert Rweyemamu
“Ujenzi wa jengo jipya la ghorofa tano kwenye eneo hili utakua mkombozi kwa wananchi ambao wana imani na huduma zinazotolewa katika Kituo cha Afya Kaloleni, mchakato umeanza na ujenzi utagharamiwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri,” amesema Kayombo.
Waziri Mchengerwa, baada ya kukagua vifaatiba vya kisasa na kuridhishwa na uboreshaji wa huduma zinazotolewa, ameagiza kituo hicho kipandishwe hadhi kuwa hospitali ya wilaya hatua itakayoifanya Jiji la Arusha kuwa na hospitali mbili za wilaya.
Amesema uwepo wa vifaatiba vya kisasa ambavyo havipatikani kwenye baadhi ya hospitali za wilaya na huduma zinazotolewa unakifanya kituo hicho kiwe na hadhi ya kuwa hospitali ya wilaya hatua itakayopanua wigo wa utendaji kazi wake na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na haraka.
Kuhusu uhaba wa watumishi 40 katika kituo hicho ameahidi kulifanyia kazi na kumwagiza Mkurugenzi wa Jiji kuajiri watumishi wa afya kwa ajira za muda hadi ufumbuzi wa kudumu utakapopatikana.
Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk Maduhu Nindwa amesema uwepo wa vifaatiba vya kisasa umeongeza maradufu idadi ya wagonjwa na hospitali imekuwa ikipata mapato ya Sh61 milioni kila mwezi sawa na Sh741 milioni kwa mwaka.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa amesema hatavumilia ukosefu wa dawa kwenye taasisi za afya za Serikali kwa sababu Bohari ya Dawa (MSD) ina uwezo wa kuhudumia hospitali, vituo vya afya na zahanati na kuonya tabia ya baadhi ya madaktari wanaomiliki maduka ya dawa kuwaelekeza wagonjwa kununua dawa huko, badala ya maduka ya Serikali.
“Hii tabia ya baadhi ya madaktari wasio waaminifu sitaivumilia, Serikali kupitia MSD ina uwezo wa kutoa dawa zinazohitajika kwenye hospitali zote za Serikali, ninazo taarifa za daktari mmoja katika Hospitali ya Temeke mwenye duka la dawa jirani na hospitali namwagiza alitoe mara moja kabla sijamtoa yeye,” amesema Mchengerwa.