Musoma. Serikali imedhamiria kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakwaza Watanzania wengi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji.
Hatua hiyo imeonekana kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), ambayo imezindua dawati maalumu la huduma mkoani Mara, likilenga kusogeza huduma karibu na wananchi, ikiwamo kuwafikia wadau wa maeneo ya vijijini ili kuongeza uelewa kuhusu fursa na majukumu ya mamlaka hiyo.
Wakizungumza mjini Musoma baada ya uzinduzi wa dawati hilo, baadhi ya wafanyabiashara na wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema ni wakati muafaka kwa Serikali kuhakikisha mikakati na programu zake zinawahusisha pia wakazi wa vijijini, badala ya kuelekezwa zaidi mijini kama ilivyozoeleka.
Mmoja wa wakazi hao, Annastazia Omollo, amesema baada ya kupata elimu kuhusu majukumu ya Tiseza, amesema kuwa emegundua kuwa wananchi wengi wa vijijini hukosa fursa mbalimbali za kiuchumi kutokana na kutofikiwa na programu za Serikali.
“Tiseza inahamasisha uwekezaji wa ndani, na ukiangalia vijijini kuna fursa nyingi sana. Kuna wafugaji na wakulima wengi wanafanya shughuli zao kwa mazoea kutokana na ukosefu wa elimu. Ni muhimu Tiseza ikawa taasisi jumuishi inayowafikia wakazi wa mijini na vijijini,” amesema.
Ameongeza kuwa wapo wafugaji wengi vijijini wanaomiliki idadi kubwa ya mifugo, lakini kutokana na kutumia mbinu za kizamani, hawapati faida inayostahili. Kwa maoni yake, endapo wafugaji hao watapatiwa elimu na mwongozo sahihi, wanaweza kubadili mifumo yao ya uzalishaji na hatimaye kuwa miongoni mwa wawekezaji wa ndani.
Kwa upande wake, Jerimia Dishon amesema vijijini kuna wafugaji wanaomiliki zaidi ya ng’ombe 200, lakini hukosa uelewa wa namna ya kugeuza rasilimali walizonazo kuwa uwekezaji wa kimkakati.
Baadhi ya wafanyabiashara wa mjini Musoma wakiwa kwenye uzinduzi wa dawati maalum la Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Tiseza) mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
“Tumeambiwa Tiseza inahusisha usajili wa miradi. Hawa wafugaji hawakosi mitaji, bali wanakosa elimu. Wakiwa na mifugo na ardhi waliyonayo, wanaweza kuanzisha miradi mikubwa ya ufugaji wa kisasa, kuongeza uzalishaji, mnyororo wa thamani na hata fursa za ajira,” amesema.
Awali, akizindua dawati hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Tiseza, Balozi Dk Aziz Mlima, amesema mamlaka hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kutumia kikamilifu fursa za uwekezaji kwa kuwapa unafuu wa kodi na mitaji.
Amesema Serikali imelenga kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani kadri iwezekanavyo, na baada ya kubaini changamoto zinazowazuia Watanzania kuwekeza, imechukua hatua za makusudi kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwahamasisha kushiriki zaidi katika shughuli za kiuchumi.
Dk Mlima amesema unafuu unaotolewa kupitia Tiseza unajumuisha misamaha ya baadhi ya kodi kwa asilimia 100 pamoja na punguzo la ushuru wa forodha kwa asilimia 75 kwa baadhi ya bidhaa, hatua inayolenga kuwasaidia wawekezaji wenye mitaji midogo na ya kati.
“Anaweza kuwepo mwekezaji ambaye mradi wake una thamani ya zaidi ya Sh2 bilioni, lakini baada ya kujisajili Tiseza, akatumia Sh1.2 bilioni tu kuanzisha mradi huo. Huu ni ushahidi wa unafuu uliopo. Nawahimiza wakazi wa Mara kutumia fursa hii kupitia dawati hili kusajili miradi yao ili tuanze kuwekeza zaidi katika mkoa wetu na nchi kwa ujumla,” amesema.
Ameeleza kuwa dawati hilo lina majukumu ya kutoa elimu kuhusu kazi na majukumu ya Tiseza, kusaidia usajili wa miradi, pamoja na kuwaelekeza wawekezaji kuhusu fursa zilizopo. Walengwa wakuu ni wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa pamoja na wajasiriamali.
Dk Mlima amewahakikishia Watanzania kuwa bidhaa zitakazozalishwa au kuongezewa thamani kupitia miradi ya Tiseza zitazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, akisisitiza kuwa mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa tija na ufanisi wa hali ya juu.
Amesema lengo ni kuhakikisha bidhaa hizo zinapata soko la ndani na nje ya nchi, hivyo kuinua uchumi wa wawekezaji binafsi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
