● Ni matokeo ya MoU kati ya GST na Taasisi ya KIGAM kutoka Korea ya Kusini,
● Utekelezaji wa mradi huo kugharimu Bilioni 40 za Kitanzania
● Wataalam kutoka GST kujengewa uwezo
● Wachimbaji wadogo kupatiwa Mafunzo malum
Wizara ya Madini – Mtumba
Ikiwa ni utekelezaji wa Madini Vision 2030, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewezesha kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha kisasa na kikubwa cha Teknolojia ya Madini Mkakati na muhimu pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa madini.
Hayo yamesemwa leo tarehe 26 Januari, 2026 na Waziri wa Madini, *Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)* alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe maalum wa Watu 6 kutoka nchini Korea ukiongozwa na *Bw. Seong-Jun Cho* ambaye ni Mtaalam kutoka Taasisi ya Jiosayansi na Rasilimali Madini ya Korea (KIGAM).
“*Mheshimiwa Rais* ametuelekeza sisi Wizara ya Madini kuhakikisha tunaongeza eneo la utafiti hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Mradi huu na wenzetu wa Korea Kusini unaonesha wazi dhamira na adhma ya Serikali yetu katika kufikia malengo tuliyojiwekea”
“Utekelezaji wa mradi huu ni matokeo ya makubaliano ya mashirikiano baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya KIGAM kutoka nchini Korea Kusini kupitia MoU iliyosainiwa tangu Mwaka 2024.
Waziri Mavunde pia alieleza kuwa mradi huo ambao unataraji kugharimu Woni bilioni 21.8 za Korea ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani Milioni 16.5 utahusisha kuanzishwa kwa Kituo cha Teknolojia ya Madini; uchunguzi wa pamoja wa Mfumo wa Kidijitali wa Taarifa za Rasilimali Madini; Ujenzi wa uwezo wa wataalam na Utekelezaji wa mifumo ya ESG ya madini.
Vilevile, Mhe. Mavunde alionesha kufurahishwa na programu hiyo na kuwataka wataalam kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia hiyo katika utafiti wa madini mengine kama ya metali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wachimbaji na wawekezaji.
Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa Serikali inatekeleza mradi wa kuwezesha vijana na wanawake kwenye sekta ya madini (MBT) na kuwaomba KIGAM kuangalia uwezekano wa kusaidia kujenga uwezo zaidi ili mradi huo uweze kufanikiwa ipasavyo.
“Pamoja na manufaa niliyoeleza ambayo yanatokana na mradi huu, pia utatoa fursa kwa wachimbaji wadogo kupata mafunzo maalum yatayoongeza ufanisi na tija ya shughuli zao” aliongeza Mhe. Mavunde.
Awali, akitoa wasilisho juu ya mradi huo, Msimamizi mkuu *Bw. Seong-Jun Cho* aliishukuru Serikali kwa ushirikiano inaotoa na kuahidi kwamba mradi huo ambao umejikita kwenye nikeli unakwenda kunufaisha Taifa wakati wa utekelezaji wake wa miaka 5 kutoka 2027 hadi 2031.



