Siasa, fedha kikwazo ujenzi daraja Mto Mligazi -2

Tanga. Kwa nini Daraja la Mto Mligazi linalounganisha wilaya za Bagamoyo, mkoani Pwani na Handeni Vijijini, Tanga, halijatengenezwa tangu Tanganyika ipate Uhuru (1961) licha ya kuwapo kwa sera, sheria na uongozi wa kisiasa na kiutawala?

Swali hilo limeendelea kuumiza vichwa vya wakazi wa vijiji vya Kwasunga, Miono na Kwamsisi waotegemea kivuko cha muda walichotengeneza kwa malighafi duni, ambacho kila msimu wa mvua huweka maisha yao shakani, huku shughuli za kiuchumi, elimu na huduma za kijamii zikikwama.

Kivuko kinachotumika kimetengenezwa kwa miti, mbao, magogo na udongo, malighafi inayooza baada ya muda mfupi na kubomoka, hususani msimu wa mvua.

Ingawa tatizo la kivuko hicho linajulikana kwa muda mrefu na viongozi wa kisiasa na kiutawala katika ngazi mbalimbali, ujenzi wa daraja umekuwa ukisuasua, hali inayochochewa na mchanganyiko wa changamoto za uongozi, fedha na mifumo ya uwajibikaji.

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanyika kwa miezi mitatu umebaini kuwa daraja hilo limekuwa ajenda ya kisiasa kila kipindi cha uchaguzi.

Wagombea wa udiwani na ubunge wamekuwa wakilitumia daraja hilo kama kipaumbele, lakini baada ya uchaguzi kumalizika hakuna utekelezaji.

Diwani wa zamani wa Kwasunga, Hamis Mwingwa, anakiri kuwa suala la daraja hilo lilitumika mara kadhaa kama nyenzo ya kisiasa.

“Tulikuwa ‘tukilipandisha’ kwenye mikutano ya hadhara kwa sababu lilikuwa kilio kikubwa cha wananchi. Kuna wakati alikuja mbunge Miono nilipopanda tu na karatasi kuzungumzia changamoto niliwekwa pembeni, ukweli ni kwamba halikuwa linapatiwa uzito unaostahili kwenye bajeti za utekelezaji,” anasema na kuongeza:

“Viongozi wa chini hatupati ushirikiano kutoka juu kama kwa wabunge, halmashauri hadi mkoa. Wakipata madaraka wanajisahau, wakati wa uongozi wangu nilipambana hata barabara haikuwa sawa ikabidi tuichonge tulitumia fedha za wananchi.”

Hussein Kamnama, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwasampa, kilichopo Kata ya Kwasunga, anasema halmashauri ya vijiji vitatu Kwandugwa, Kwanyanje na Kwasunga kila kimoja kilichangisha Sh1 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kivuko.

Diwani wa zamani, Mwingwa anasema kukosekana kwa uwajibikaji kutoka kwa viongozi walio madarakani kumechangia kuchelewa kwa ujenzi wa daraja la kudumu.

Katika ngazi ya kiutawala, hoja ya Daraja la Mto Mligazi imekuwa ikipita kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya wilaya bila kufikia hatua ya utekelezaji kamili.

Aliyekuwa mtendaji wa kata eneo la Kwasunga ambaye hakutaka kutajwa jina anasema mara kadhaa mapendekezo ya ujenzi wa daraja hilo yaliwasilishwa, lakini yalikwama kutokana na mabadiliko ya vipaumbele.

“Nikiwa madarakani nimeshuhudia vifo vya watu takribani sita kwa mwaka. Ukweli ni kwamba daraja ni changamoto na si kwamba mipango haikuwepo hapana, ilikuwepo. Hata ramani za awali zilishawahi kufanywa. Tatizo lilikuwa mabadiliko ya viongozi na vipaumbele vipya kila mwaka wa bajeti,” anasema.

Anaeleza hali hiyo imesababisha miradi mingine kama ya maji na umeme kupewa kipaumbele, huku daraja ambalo ndilo kikwazo kikubwa likiachwa.

Ukosefu wa fedha ni changamoto nyingine inayotajwa kukwamisha ujenzi wa daraja la kudumu.

Ujenzi wa daraja la kudumu unahitaji gharama kubwa, ikilinganishwa na vivuko vya muda ambavyo vimekuwa vikijengwa na wananchi kwa nguvu zao wenyewe.

Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), Wilaya ya Handeni, Mhandisi Judica Makyao anasema ujenzi wa Daraja la Mto Mligazi unahitaji fedha kutoka Serikali Kuu.

“Miradi kama hii inahitaji fedha nyingi. Mapato ya ndani ya halmashauri hayawezi kukidhi, hivyo bila fedha kutoka Serikali Kuu, utekelezaji unakuwa mgumu,” anasema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Tarura na miongozo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), jukumu la ujenzi na matengenezo ya madaraja ya vijijini linapaswa kutekelezwa kupitia mipango ya maendeleo ya halmashauri husika, kwa kushirikiana na Tarura na Serikali Kuu.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini licha ya Daraja la Mto Mligazi kutambuliwa kwa muda mrefu kama eneo hatarishi, bado halijawekwa kwenye utekelezaji wa mradi wa kudumu, hali inayozua maswali kuhusu uwajibikaji wa taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia miundombinu ya vijijini.

Mhandisi Makyao anasema kisheria daraja hilo liko chini ya mamlaka ya halmashauri, lakini utekelezaji wake unategemea upatikanaji wa fedha kutoka Serikali Kuu.

“Kisheria, Tarura tunatekeleza miradi kwa mujibu wa bajeti inayotengwa. Kama daraja halijaingizwa kwenye mpango wa fedha wa mwaka husika utekelezaji wake unakuwa mgumu,” anasema.

Ofisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) ambaye hakutaka kutajwa jina anasema licha ya kuwapo kwa sera na miongozo, changamoto imekuwa katika upangaji wa vipaumbele na ufuatiliaji wa miradi.

“Sera zipo, miongozo ipo, lakini utekelezaji unategemea namna halmashauri zinavyowasilisha miradi yao na kufuatilia hadi fedha zipatikane,” anasema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Vijijini, Mussa Mwanyumbu, anasema wamekuwa wakijadili suala la daraja hilo kila wanapokutana kwenye vikao vya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).

“Tunapokutana kwenye vikao viongozi wa halmashauri huwa tunazungumzia changamoto hiyo tunaambiwa tusubiri mpango wa Serikali kuna mradi wa Rise unaweza kutusaidia. Tarura wanajua hilo, walisema wamepeleka maombi makao makuu na wanasubiri majibu,” anasema.

Rise ni mradi wa uboreshaji wa barabara vijijini kwa ushirikishaji wa jamii na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi.

“Daraja hili ni kubwa na linahitaji bajeti kutoka Serikali Kuu, Tarura wanafahamu hilo tunawakumbusha tunapokutana nao kwenye vikao, lakini tuliambiwa kuna vipaumbele vingi, mfano Kwa Nyanje bado hatuna zahanati,”  anasema na kuongeza:

“Mwaka 2005 tulitengewa Sh300 milioni za ujenzi wa daraja hilo, ikaibuka changamoto ya maji wananchi walipoulizwa wakasema wawekewe maji, fedha ikahamishiwa huko.”

Mwanyumbu, diwani wa zamani wa Mkata anashauri Serikali kulipa daraja hilo hadhi ya mradi wa kimkakati.

“Nafikiri siku moja Waziri wa Ujenzi akifika kuona hali halisi litafanyiwa kazi kwa sababu hili si daraja la kijiji kimoja linaunganisha kata na wilaya mbili. Serikali ikiliweka kama mradi wa kimkakati, fedha zitapatikana,” anasema.

Diwani wa Kwasunga, Jasmini Paulo anasema: “Kama kungekuwa na daraja watu wanaotoka Dar es Salaam kwenda Handeni kungekuwa na ahueni ya nauli, mtu analipa ya kawaida, akifika Miono anatoa Sh10,000 kwa ajili ya bodaboda afikishwe hadi vijijini.”

Anaiomba Serikali iangalie suala hilo ikiwezekana mwaka huu changamoto hiyo ya muda mrefu itatuliwe.

Kwa upande wake, kiongozi wa kimila katika Kijiji cha Kwasunga, Yusuph Suleiman maarufu Kulufi, anasema kuchelewa kwa ujenzi wa daraja hilo kumeathiri si tu huduma za kijamii, bali pia ushirikiano na mawasiliano baina ya kijiiji kimoja hadi kingine wakati wa mvua.

“Watu wanashindwa hata kufika misibani au hospitali kipindi cha mvua wananchi wa Miono, Masimbani wanasimama kule na sisi wa Kwasunga, Kwakonje tunasimama huku tunasalimiana. Hili ni tatizo linalogusa utu wa jamii,” anasema na kuongeza:

“Hili linasababisha usumbufu kwenye sekta mbalimbali kama afya, elimu na kilimo, huduma ambazo wakazi wanategemea daraja hilo kufanikisha.”

Daraja la Mto Mligazi limebaki kuwa mfano halisi wa pengo kati ya sera, ahadi na utekelezaji. Bila uwajibikaji wa wazi wa kisiasa, kiutawala na kifedha, wakazi wa Handeni Vijijini wataendelea kuhatarisha maisha yao kila msimu wa mvua.

Swali linabaki kuwa, daraja hilo litaendelea kuwa ahadi ya kampeni au hatimaye litageuka kuwa mradi wa kudumu unaookoa maisha na kukuza uchumi wa wananchi.