Stanbic yajivunia kuwa mshirika muhimu taasisi za fedha nchini

Dar es Salaam. Kadiri Tanzania inavyoendelea kupanua na kuimarisha masoko yake ya mitaji, bidhaa za kifedha ambazo kwa muda mrefu zilihusishwa zaidi na taasisi kubwa sasa zinaanza kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Hatua hiyo inaonekana wazi kupitia utoaji wa hivi karibuni wa Sukuk ya Al Barakah ya Benki ya CRDB, ambayo imechukuliwa kama ishara muhimu ya kukua kwa masoko ya mitaji na upanuzi wa fursa za uwekezaji kwa wananchi wa kawaida.

Katika mchakato huo, Benki ya Stanbic ilishiriki kama mshirika mwenza wa upangaji wa Sukuk hiyo, ikitoa mchango wake wa kitaalamu katika maandalizi, upangaji na utekelezaji wa muamala mzima. Ushiriki huo umeiwezesha Sukuk ya CRDB kutekelezwa kwa ufanisi, huku ikizingatia viwango vya kitaalamu na matarajio ya wawekezaji.

Hii ni awamu ya tatu ambapo Stanbic imehusika katika kuipangilia Sukuk ya CRDB, hali inayoonesha kuimarika kwa uzoefu na uwezo wa taasisi za kifedha nchini katika kuandaa na kusimamia bidhaa za uwekezaji za kisasa.

Akizungumza juzi, Januari 24, 2026, Makamu wa Rais Mwandamizi wa Benki ya Stanbic anayesimamia Masoko ya Mitaji Afrika Mashariki, Sarah Mkiramweni, amesema mafanikio ya Sukuk hiyo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Benki ya Stanbic, wapangaji wengine pamoja na wadhibiti wa sekta ya fedha.

Ameongeza kuwa vyombo vya kifedha vinavyoungwa mkono na mali halisi, kama ilivyo kwa Sukuk, vina nafasi kubwa ya kuimarisha masoko ya mitaji na kupanua wigo wa uwekezaji kwa wananchi, sambamba na kukuza uelewa wa umma kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya fedha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Ester Manase, amesema mafanikio ya Sukuk ya CRDB yanaonesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika bidhaa za kifedha zinazotolewa sokoni.

Amesema ushauri wa kitaalamu, maandalizi ya nyaraka kwa viwango vinavyotakiwa, pamoja na uhamasishaji wa wawekezaji, ni nguzo muhimu katika kuhakikisha bidhaa kama Sukuk zinaeleweka na kukubalika kwa urahisi.

Amesisitiza kuwa mchango wa Benki ya Stanbic hauishii kwenye Sukuk ya CRDB pekee, bali pia benki hiyo imehusika katika upangaji wa dhamana za miundombinu, dhamana za kijani, pamoja na mikopo mikubwa ya pamoja inayolenga kuunga mkono ajenda za maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa Manase, hatua hizo zinasaidia kuelekeza mitaji kwenye miradi ya maendeleo inayochangia uanzishaji wa ajira, uboreshaji wa huduma za jamii na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa ujumla, hivyo kuifanya sekta ya fedha kuwa chachu muhimu ya maendeleo endelevu nchini.