::::::
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), imesema kabla ya kutangaza utabiri wake wa mvua, imekuwa ikifanya vikao vya ushauri na wadau pamoja na taasisi za Serikali ili kupata maoni ya kisekta.
Akizungumza na Torch Media katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Alfred Kondoya, amesema mchakato huo ni sehemu ya maandalizi muhimu ya kuhakikisha utabiri unaotolewa unakuwa sahihi na wenye manufaa kwa jamii.
Kondoya amesema vikao hivyo huwakutanisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali zikiwemo wizara ya maji, kilimo, nishati na miundombinu, ili kubaini mahitaji na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.
Ameeleza kuwa taasisi zinazoshirikishwa ni pamoja na Wizara ya Maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wadau wengine wa umma na binafsi.
Kwa mujibu wa Kondoya, ushirikishwaji wa wadau husaidia TMA kutoa utabiri unaozingatia hali halisi ya maeneo husika na kutoa ushauri unaolenga kupunguza athari za mvua nyingi au upungufu wa mvua.
Ameongeza kuwa utabiri wa mvua za Masika unatarajiwa kutangazwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu na utahusu kipindi cha kuanzia mwezi Machi hadi Mei.
TMA imewataka wananchi na wadau kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa zitakazotolewa na mamlaka hiyo kupitia vyombo vya habari na mitandao yake rasmi.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa ni muhimu katika kulinda maisha, mali na kusaidia mipango endelevu ya maendeleo nchini.