:::::::::
Na Mwandishi Wetu
TMA imesema inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za Masika mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, utabiri ambao utahusu kipindi cha kuanzia mwezi Machi hadi Mei.
Akizungumza na Torch Media katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Alfred Kondoya, amesema utabiri huo ni muhimu kwa mipango ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, maji, nishati na miundombinu.
Kondoya amesema utabiri wa mvua za Masika huwa na mchango mkubwa katika kusaidia Serikali, wadau na wananchi kupanga shughuli zao za maendeleo na kiuchumi kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya hewa unaotarajiwa.
Amesema kutokana na umuhimu wake, wananchi wanapaswa kuwa wavumilivu na kusubiri tangazo rasmi la TMA ili kupata mwelekeo sahihi wa msimu wa Masika badala ya kutegemea taarifa zisizo rasmi.
Aidha, TMA imesema kabla ya kutangaza utabiri huo, huwa inafanya maandalizi ya kina ikiwemo ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za hali ya hewa kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa mamlaka hiyo pia hufanya vikao vya ushauri na taasisi za Serikali pamoja na wadau muhimu ili kuhakikisha utabiri unaotolewa unazingatia mahitaji ya sekta husika.
Baadhi ya taasisi zinazoshirikishwa katika mchakato huo ni pamoja na Wizara ya Maji, DAWASA, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi nyingine za umma na binafsi.
Kwa mujibu wa TMA, ushirikishwaji wa wadau hulenga kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa.