Simiyu. Wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamehimizwa kutumia misaada ya kisheria inayotolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kujua haki zao na kutatua migogoro kwa njia ya amani inapojitokeza.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Januari 26, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanzishwa kwa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa itakayoshughulikia migogoro kati ya Serikali na wananchi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa haki na elimu ya kisheria, huku wananchi wakitakiwa kushiriki kliniki ya kisheria itakayofanyika kuanzia Februari 2 hadi 8, 2025 katika wilaya zote za Mkoa wa Simiyu.
“Kamati hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria bila malipo, hususan katika migogoro dhidi ya Serikali na masuala mengine ikiwemo migogoro ya mirathi,” amesema Macha.
Watumishi wa kada mbalimbali katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye mkutano wa Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anamringi Macha (hayupo pichani). Picha na Samwel Mwanga
Amebainisha kuwa wananchi wengi hukumbwa na changamoto za kisheria lakini hukosa uelewa wa njia sahihi za kudai haki zao, hali inayosababisha kupoteza haki za msingi.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Silinde Mmada, amesema elimu ya kisheria ni nyenzo muhimu katika kutatua migogoro na kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa.
Amesema kuanzishwa kwa kliniki za kisheria zisizotoza gharama kutawawezesha wananchi, hususan wasiokuwa na uwezo wa kumudu huduma za kisheria, kupata haki kwa usawa.
“Jamii yenye uelewa wa kisheria hupunguza migogoro isiyo ya lazima na kuvutia wawekezaji, jambo linalochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema.
Baadhi ya wananchi wa mkoa huo wamepongeza mpango huo. Mkazi wa Maswa, Sylvester Lugembe, amesema migogoro ya mirathi imekuwa chanzo cha chuki katika familia nyingi, huku Fatuma Hassan wa Somanda, Bariadi, akisema ushauri wa kisheria bila malipo utawasaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wao kabla ya kukimbilia mahakamani.