Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wamelalamikia kelele kubwa zinazofanywa na madereva bodaboda kwa kufunga honi zenye sauti ya juu pamoja na kutengeneza mlio mithili ya mlipuko wa bomu ambao umekuwa ukiwashtua.
Malalamiko hayo yametokana na kukithiri kwa tabia hiyo ya vijana waliojiajiri kuendesha bodaboda kupiga honi hizo pamoja na ‘kulipua’ bila sababu zozote za msingi huku wenyewe wakifurahia wanachokifanya.
Kiongozi wa waendesha bodaboda nchini anakiri kuwepo kwa malalamiko hayo huku akisema changamoto hiyo inasababishwa na kukosekana kwa usimamizi bora wa sheria utakaowalazimisha vijana kufuata utaratibu wa usalama barabarani.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limebainisha kwamba, tatizo hilo limekuwa likisababishwa na vijana wenye ujana uliopitiliza ambao wamekuwa wakifanya doria mara kwa mara kuwakamata vijana wenye tabia hatarishi.
Mkazi wa Buguruni, Asha Mussa akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Januari 26, 2026 amesema kelele hizo huwa zinamkera hasa akiwa anatembea barabarani, jambo ambalo linaweza kusababisha ajali.
“Mara ya kwanza nilidhani ni gari linakuja kunigonga. Niliposhtuka, nikakuta ni bodaboda tu imepiga honi, mlio ulikuwa mkubwa kama gari aina ya lori,” amesimulia.
Amesema sauti hizo zimekuwa zikiwakwaza wanajamii hasa wagonjwa, watoto na wazee kususani nyakati za asubuhi na usiku. Amesema hali hiyo inasababisha hofu, usumbufu na hata ajali.
Mzee Juma, mkazi wa Tabata, amesema tabia hiyo imekuwa kero ya kila siku hasa asubuhi na jioni na wengine wamekuwa wakifanya mashindano, hawajali kabisa watu wenye maradhi au wazee.
“Wapo wanafanya makusudi, wanabonyeza honi mfululizo ili watu wawapishe haraka. Lakini sauti inakuwa ni kali kupita kiasi, inachanganya. Unasikia honi kali ghafla unadhani ni gari kubwa au ajali imetokea. Moyo unaruka,” amesema.
Amesema maeneo ya mataa mengi gari zikizuiwa kwa muda pale zinapoachiwa huwa wanapiga honi za kila aina kana kwamba kundi hilo la wasafiri limeshindikana na haliwezi kudhibitiwa.
Buguruni na Tabata zinawakilisha maeneo mengi nchini, wananchi wanalalamikia hali hiyo, jambo ambalo wamedai linahitaji uangalizi wa karibu utakaowezesha kuondokana na hali hiyo.
Akizungumzia jambo hilo, dereva wa pikipiki, Juma Salum amekiri kwamba baadhi ya madereva wenzake hufanya hivyo makusudi.
“Wanafanya hivyo ili watu waogope na wawapishe haraka, lakini hawajui madhara yake kwa jamii,” amesema.
Amesema hiyo inaitwa “stop injini” na baadhi wanabadilisha mifumo kama fasheni na kwenda kwa mafundi kufunga honi wanazotaka huku akisema hakuna kipingamizi.
“Unajua ukifika kwa fundi unataka kufunga honi, mafundi wanakuuliza unataka kufunga honi aina gani, Land Cruiser Prado ama? Unachochagua wanakufungia,” amesema Salum.
Mwenyekiti wa Bodaboda na Bajaji nchini, Said Kagomba amesema usugu wa tatizo hilo ni usimamizi wa sheria na kila dereva awapo barabarani lazima azingatie utaratibu wa usalama barabarani.
“Hapa waulizwe polisi wa usalama barabarani, wao wanasimamia sheria, inakuwaje tatizo hili linakuwa kubwa, na si honi na kuongeza mifumo ya sauti kuna watu wanabeba mishikaki watu zaidi ya wanne,” amesema.
Kagomba amesema kuangalia honi na mifumo ya sauti haitoshi, bali kuna matatizo mengine matatu ambayo ni kero, kwa kuwa baadhi ya bodaboda wanakaa sehemu za zebra.
“Watu wamekuwa wakitoa ‘sight mirror’ na hawavai kofia, shirikisho limesimama kutoa elimu kwa madereva wote wa pikipiki wajue wajibu wao wawapo barabarani lakini hawafanyi,” amesema.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Kitengo cha Usalama Barabarani, William Mkonda amesema Jeshi la Polisi limekuwa likifanya operesheni za mara kwa mara kukamata pikipiki zinazofanya michezo hatarishi na kusababisha kelele barabarani.
Mkonda amesema tatizo hilo ni kubwa katika miji mikubwa na limechangiwa zaidi na vijana wenye ujana uliopitiliza ambao wengi wao wanafahamu kuwa, wanachokifanya ni kinyume cha sheria, lakini hukiona kama fahari kutokana na kelele kubwa za pikipiki zao.
Amesema katika kusimamia sheria, polisi wamekuwa wakilifanyia kazi suala hilo kwa umakini zaidi, hasa katika Jiji la Dar es Salaam na miji mingine kama Arusha, sambamba na kutoa elimu kwa wahusika.
“Tunaendelea kutoa elimu kuhusu athari za vitendo hivyo kwa kushirikiana na vyama vya waendesha pikipiki na bajaji vya kitaifa vilivyopo Dar es Salaam na mikoa mingine,” amesema Mkonda.
Amesema viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakitoa ushauri siyo tu kuhusu kelele hizo, bali pia makosa mengine yanayofanywa na kundi la usafirishaji, huku akieleza wanatarajia mafanikio kutokana na ushirikiano uliopo.
