Zanzibar yapokea mabasi mapya ya umeme

Unguja. Awamu ya kwanza ya mabasi yanayotumia umeme (ZanBus) yamewasili kupitia Bandari ya Malindi, Zanzibar.

Mabasi hayo 10, yamewasili jana Januari 25, 2026 katika Bandari ya Malindi na kuelekea katika maegesho ya stendi mpya ya Kijangwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zanzibar, leo Januari 26, 2026 imeeleza mabasi hayo yanatarajiwa kuanza kutoa huduma rasmi za usafiri wa abiria Februari 2026.

Mabasi mapya ya umeme yakiwa barabarabii kuelekea katika maegesho ya stendi mpya ya Kijangwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Hatua hiyo inayolenga kupunguza msongamano wa magari barabarani pamoja na kuboresha usafiri rafiki kwa mazingira Zanzibar,” amesema.

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Raqey Mohamed amesema mradi huo, unaotarajiwa kuendelea kutekelezwa hatua kwa hatua, unaratibiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na utasimamiwa na Kampuni ya Usafirishaji ya Unitrans kutoka Afrika Kusini.

Mabasi mapya ya umeme yakiwa barabarabii kuelekea katika maegesho ya stendi mpya ya Kijangwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mradi wa mabasi ya umeme (ZanBus) ni sehemu ya juhudi za Serikali ya awamu ya nane ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi.

Kwa hatua za mwanzo, mabasi hayo yanatarajia kutumiwa katika njia za Buyu, Chukwani, Mnazimmoja hadi Malindi na mengine kutoka Uwanja wa Ndege hadi Malindi.