Morogoro. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Ebenezeri Mbwambo (34), mkazi wa Morogoro, anadaiwa kujinyonga ndani ya chumba alichokodi katika nyumba ya kulala wageni ya Kisenga, iliyopo mtaa wa Ngyzo, kata ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema tukio hilo lilibainika baada ya muhudumu wa nyumba hiyo kugundua damu na maji yakitoka chini ya mlango wa chumba namba 106, hali iliyosababisha kutoa taarifa polisi na baadaye mlango kuvunjwa kwa kufuata taratibu.
Amesema uchunguzi wa awali na vielelezo vilivyokutwa ndani ya chumba vinaashiria kuwa marehemu alijidhuru kwa kutumia kitu chenye makali, akiwa katika hali ya ulevi, huku akijifungia mlango kwa ndani, ingawa uchunguzi wa kina bado unaendelea.
Aidha, imeelezwa kuwa marehemu aliingia katika nyumba hiyo ya kulala wageni Januari 26,2025 saa moja usiku akiwa na begi, na kabla ya kwenda kulala alionekana akinywa pombe katika baa iliyopo ndani ya eneo hilo.
Kwa upande wake, mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni, Kilinga Pololeti, amesema tukio hilo ni la kwanza kutokea katika eneo hilo. Mkazi wa eneo hilo, Nurdin Mtamike, ameshauri kuwekwa kwa mifumo ya usalama ikiwemo kamera, mlango wa dharura na ulinzi madhubuti ili kuzuia au kubaini mapema matukio ya aina hiyo.