Tanga. Licha ya kuwapo sheria zinazoelekeza wazi, ni wajibu wa Serikali katika ujenzi na usimamizi wa barabara na madaraja ya vijijini, wakazi wa vijiji vya Kwasunga, Kwamsisi na Miono, wilayani Handeni wanaendelea kuishi katika hatari ya vivuko visivyo salama kila msimu wa mvua.
Uchunguzi wa miezi mitatu uliofanywa na Mwananchi, umebaini kuwa tatizo la daraja la Mto Mligazi halitokani na ukosefu wa sheria, sera au utaalamu wa ujenzi, bali ni udhaifu wa utekelezaji, ucheleweshaji wa fedha na vipaumbele vinavyowaacha wananchi wakilipa gharama kwa maisha yao, elimu ya watoto na shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Barabara Tanzania ya mwaka 2007 (Sura ya 13), mamlaka za barabara zinatakiwa kuhakikisha upatikanaji salama wa barabara, madaraja na njia za mawasiliano, hususani katika maeneo ya vijijini.
Hata hivyo, pamoja na masharti mengine ya sheria hiyo yanayohusu upangaji wa matengenezo, idhini za ujenzi na bajeti ya miundombinu, utekelezaji wake katika baadhi ya maeneo ya vijijini umeendelea kuwa changamoto.
Vilevile, kifungu cha 9(2) cha sheria hiyo kinakataza ujenzi wa miundombinu ya barabara au madaraja bila idhini ya mamlaka husika, wakati kifungu cha 12 kinazitaka mamlaka za barabara kuwa na mipango ya matengenezo pamoja na bajeti ya kudumu kwa ajili ya barabara na madaraja ya vijijini.
Licha ya sheria hizo, vivuko vya muda vimeendelea kutumika kwa muda mrefu bila mpango wa kudumu wa ujenzi wa daraja salama.
Vilevile, Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 pamoja na Kanuni za Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) za mwaka 2017 zinawataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kuwa, miundombinu yote inajengwa na kutunzwa kwa kuzingatia usalama, viwango vya kitaifa na tathmini za athari za mazingira kabla ya utekelezaji.
Hata hivyo, kwa wananchi wa Handeni Vijijini, utekelezaji wa matakwa hayo ya kisheria umeendelea kuwa hafifu.
Ripoti ya Tarura ya mwaka 2023 inaonesha kuwa, zaidi ya madaraja 1,200 ya vijijini nchini yako katika hali hatarishi kutokana na matumizi ya mbao na vifaa visivyoidhinishwa katika ujenzi, hali inayochangia ajali na kuongeza gharama za matengenezo.
Mbali ya hayo, utafiti wa Shirika la JICA wa mwaka 2021 kuhusu matengenezo ya barabara za wilaya, umebaini kuwa, zaidi ya asilimia 40 ya maeneo ya vijijini nchini hukatika mawasiliano kwa siku kati ya 30 hadi 90 kila msimu wa mvua kutokana na uwepo wa madaraja yasiyo rasmi.
Kwa muktadha huo, changamoto ya daraja la Mto Mligazi haionekani kuwa ni matokeo ya ukosefu wa sheria au miongozo, bali ni udhaifu wa utekelezaji, usimamizi na ufuatiliaji wa majukumu ya taasisi husika.
Kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 9), nchi wanachama zinapaswa kuwekeza katika miundombinu salama na imara ili kuunganisha jamii na huduma muhimu.
Madaraja ya vijijini yanatajwa kuwa sehemu muhimu ya maendeleo na ustawi wa wananchi.
Vilevile, miongozo ya Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inaelekeza kuwa vivuko vya muda vinapaswa kuwa suluhisho la dharura la muda mfupi na si mbadala wa madaraja ya kudumu, hususani katika maeneo yanayokatwa mawasiliano kila msimu wa mvua.
Kwa mtazamo wa kimataifa, ucheleweshaji wa ujenzi wa madaraja ya vijijini unachukuliwa kama hatari na nchi zinahimizwa kutekeleza miradi ya miundombinu kwa bajeti za uhakika na za zaidi ya mwaka mmoja ili kuepuka athari kwa wananchi.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, ujenzi wa madaraja ya vijijini unawezekana pale ambako miradi inapewa kipaumbele na kusimamiwa kwa karibu.
Kupitia mradi wa uboreshaji wa barabara vijijini kwa ushirikishaji wa jamii na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi (Rise), baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga yamejenga na kuboresha madaraja na makalavati yaliyokuwa yakisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wakati wa mvua.
Katika Wilaya ya Handeni, ikiwamo Kata ya Kilindi na Tanga Mjini, miradi ya Rise imetekeleza ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja, hatua iliyorahisisha usafiri wa wananchi, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na elimu, pamoja na kuchochea shughuli za kilimo na biashara.
Mafanikio hayo yamekuja baada ya miradi hiyo kupewa uzito wa kimkakati, kutengewa bajeti maalumu na kusimamiwa kwa ukaribu na Tarura kwa kushirikiana na halmashauri na Serikali ya mkoa.
“Kuna madaraja kama Mto Msambazi –Kwediboma, Magamba –Kwedikazu hadi Segera yalikuwa na changamoto kubwa lakini sasa wanafunzi wanakwenda shule na huduma za kijamii zinapatikana,” anasema Meneja wa Tarura, Wilaya ya Handeni, Mhandisi Judica Makyao.
Mtaalamu wa Majengo na Miundombinu, Mhandisi Milton Nyerere anasema changamoto kubwa ya miradi mingi ya miundombinu si ukosefu wa mipango, bali ni bajeti zisizo halisia na ucheleweshaji wa fedha.
“Bajeti nyingi zinazopitishwa si za kweli. Fedha hazifiki kwa wakati, malipo yanachelewa wakati mwingine kwa miezi kadhaa, wakati kitaalamu fedha zinapaswa kupatikana ndani ya mwezi mmoja au chini ya hapo,” anasema.
Anabainisha kuwa Tarura na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) hufanya kazi ya kuandaa na kutekeleza miradi, lakini changamoto hujitokeza pale fedha zinapochelewa kutolewa.
“Mwisho wa siku anayeumia ni mwananchi wa kawaida. Mradi unasimama, vivuko vinabomoka na wananchi wanaendelea kuhatarisha maisha yao, nimejaribu kuzungumzia iwepo akaunti maalumu kwa ajili ya mradi fulani hilo halitaleta usumbufu, nakumbuka zamani bajeti ilikuwa inatengwa moja kwa moja kwa hiyo Tarura au Tanroads wanakuwa hawapati tabu,” anasema.
Mtaalamu wa barabara, Fredy Nyenga anasema miradi ya miundombinu ya vijijini haipaswi kuendelea kutegemea misaada ya nje, wakati rasilimali na uwezo vipo ndani ya nchi.
“Hatuwezi kusema tusubiri msaada wa nje rasilimali zipo humu ndani. Ukishakuwa na mipango, wataalamu, mashine na vifaa, hakuna kinachoshindikana,” anasema.
Nyenga anaeleza kuwa, barabara na madaraja ni kipaumbele cha msingi kwa maendeleo ya jamii.
“Barabara ni kipaumbele hakuna kipingamizi watu wa kujenga wapo, mashine zipo zamani madaraja yalichelewa kujengwa kwa sababu tulisubiri rasilimali kutoka nje, kwa nini sasa ishindikane ilihali tuna kila kitu shida? Hapo ni fedha tu,” anasema.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa, daraja la Mto Mligazi si tatizo la ukosefu wa sheria, sera au utaalamu ni tatizo la utekelezaji, vipaumbele na uwajibikaji.
Serikali Kuu inabaki na jukumu la kutenga bajeti inayolingana na ukubwa wa tatizo. Tarura ina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kitaalamu, huku Serikali ya mkoa na halmashauri zikiwajibika kufuatilia na kusukuma mradi huo kwa ukaribu.
Bila ya kuchukuliwa hatua za haraka, daraja la Mto Mligazi na mengine wilayani humo yataendelea kuwa changamoto kubwa kwa wananchi.