Fao la utengamao lawainua wafanyakazi waliopata ajali kazini

Arusha. Wafanyakazi wanaopata ajali au magonjwa yatokanayo na kazi zao wataanza kunufaika na Fao la Utengamao kupitia mafunzo ya ujuzi na stadi mbalimbali zitakazowawezesha kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dk John Mduma, jana Jumatatu Januari 26, 2026, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa watoa huduma za utengamao kutoka mikoa saba nchini, yanayofanyika jijini Arusha.

Dk Mduma amesema jukumu la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata ajali kazini au magonjwa yatokanayo na kazi zao, kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263.

“WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa lengo la kuhakikisha wafanyakazi wanaolipata janga kazini wanapata haki zao kwa wakati,” amesema.

Ameeleza kuwa mfuko huo unatoa jumla ya mafao saba, ambayo ni huduma za matibabu, malipo ya ulemavu wa muda, malipo ya ulemavu wa kudumu, huduma za utengamao, msaada wa mazishi, malipo kwa wategemezi wa mfanyakazi aliyefariki dunia kutokana na kazi na malipo kwa mtu anayemsaidia mgonjwa.

Dk Mduma ameongeza kuwa Fao la Utengamao limegawanyika katika makundi matatu, ambayo ni utengamao wa kitabibu, mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi pamoja na utengamao wa kijamii.

“Malengo ya huduma hizi ni kumrejeshea mhanga uwezo wa kibailojia wa viungo vilivyoathiriwa, kumwezesha kushiriki katika shughuli za kujipatia kipato na kumrudisha katika maisha ya kawaida ya kijamii,” amesema.

Ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa huduma hizo, WCF imeamua kuwajengea uwezo watoa huduma za utengamao nchini ili kuhakikisha wanazitoa kwa kuzingatia taratibu na vigezo vinavyohitajika.

Kwa mujibu wa Dk Mduma, jumla ya watoa huduma 186 wamekwisha kunufaika na mafunzo hayo katika awamu mbili zilizopita, huku awamu ya sasa ikiwajumuisha watoa huduma 100 kutoka mikoa ya Tanga, Mwanza, Dodoma, Kilimanjaro, Singida, Manyara na Arusha.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa WCF, Dk Abdulsalaam Omar, amesema mafunzo hayo yanalenga kumpa mfanyakazi ujuzi mbadala na vifaa saidizi kulingana na ulemavu alioupata ili aweze kuendelea kushiriki katika jamii.