Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba, imefuta uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Bukoba na kuruhusu rufaa iliyowasilishwa na Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.
Rufaa hiyo ya ardhi namba 28882/2024 ilikatwa na Bodi ya Wadhamini hao dhidi ya Clemence Jeremiah.
Mgogoro huo wa ardhi ulitokana na madai ya umiliki wa ardhi iliyokuwa ikitumiwa na Kituo cha Watoto cha Tumaini (ELCT), kinachotoa huduma za malezi na hifadhi kwa watoto walio katika mazingira magumu,kilichopo chini ya dayosisi hiyo.
Clemence alidai kuwa ardhi hiyo ni mali yake halali na kwamba kituo hicho kilikuwa kinazuia matumizi yake, suala lililowasilishwa katika Baraza la Kata ya Nyanga kwa ajili ya upatanishi kama inavyotakiwa na sheria.
Hata hivyo, baraza hilo lilitoa hati iliyoitwa Cheti cha Usuluhishi, ambacho kilieleza wazi kuwa Clemence ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo na kutoa maelekezo dhidi ya Kituo cha Watoto cha Tumaini, ikiwemo kuondoa walinzi waliokuwepo eneo hilo.
Baada ya uamuzi huo, shauri liliwasilishwa Baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Bukoba,ambapo baraza hilo lilitupilia mbali maombi ya KKKT kwa hoja kuwa halikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni suluhu iliyopatikana katika Baraza la Kata.
Katika rufaa ya sasa, Bodi hiyo ilikuwa na sababu tatu ambazo ni Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya lilikosea kisheria kwa kushindwa kutathmini ipasavyo uhalali wa cheti kilichotolewa na Baraza la Kata, pamoja na kushindwa kutumia mamlaka yake ya marekebisho licha ya ukiukwaji wa wazi wa sheria.
Upande wa mrufani uliwasilishwa na Wakili Lameck Erasto, wakati mjibu rufaa aliwakilishwa na Wakili Pilly Hussein na pande zote ziliwasilisha hoja zao kwa maandishi.
Uamuzi wa Rufaa hiyo umetolewa jana Januari 26,2026 na Jaji Gabriel Malata,na nakala ya uamuzi huo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Baada ya kupitia hoja za pande zote na mwenendo wa shauri hilo, Jaji Malata amesema kuwa Mahakama inafuta uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kwani ni batili na lilikosa mamlaka kisheria.
“Hakukuwa na mkataba wa usuluhishi uliofikiwa,kurekodiwa na kusainiwa na pande zilizohusika katika mgogoro huo hivyo rufaa inaruhusiwa kwa amri kwamba Baraza liliendelea kusikiliza kesi bila mamlaka.”
Jaji amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Baraza la Kata lina mamlaka ya kupatanisha tu, na si kutoa uamuzi wa lazima kuhusu umiliki wa ardhi.
Mahakama ilibainisha kuwa kile kilichotolewa na Baraza la Kata ya Nyanga hakikuwa upatanishi halali kwa sababu hakukuwa na makubaliano ya usuluhishi yaliyosainiwa na pande zote, wala hakukuwa na utaratibu wa upatanishi uliorekodiwa kama inavyotakiwa na Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi.
Mahakama ilisema cheti hicho kilikuwa na maelezo yanayoonyesha wazi uamuzi wa upande mmoja, ikiwemo kauli kwamba Clemence ndiye mmiliki halali wa ardhi na kwamba Kituo cha Watoto cha Tumaini kiondoe walinzi wake.
“Mahakama inaamuru mgogoro urudishwe Baraza la Kata ya Nyanga kwa ajili ya upatanishi kwa kufuata kikamilifu sheria na ikiwa mkataba wa usuluhishi na upatanishi wa mgogoro utafikiwa, unapaswa kuwa na masharti ya usuluhisi wa mgogoro na kusainiwa na pande zote mbili,”amesema
Awali Wakili Lameck aliyemwakilisha mrufani, aliiomba Mahakama Kuu ibatilishe uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, akidai kuwa baraza hilo lilijiongezea mamlaka kinyume cha sheria.
Hoja nyingine zilikuwa cheti cha Baraza la Kata ya Nyanga, hakikuwa upatanishi halali na kudai halikufanya upatanishi kama sheria inavyotaka, bali lilitoa uamuzi wa moja kwa moja wa kumtangaza Clemence kuwa mmiliki wa ardhi.
Alidai kwa mujibu wa sheria, Baraza la Kata lina mamlaka ya kupatanisha tu, si kuamua umiliki wa ardhi na hakukuwa na makubaliano ya kusainiwa na pande zote, akisisitiza hakuna mkataba wa usuluhishi uliosainiwa na pande zote, jambo linalofanya kile kilichoitwa “Cheti cha Usuluhishi” kuwa batili kisheria.
Wakili huyo alidai kulikuwa na kasoro za kiutaratibu, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya lilipaswa kuzingatia haki ya msingi ya kusikiliza mgogoro wa ardhi na kuwa lilipaswa kutumia mamlaka ya marekebisho na kuomba rufaa iruhusiwe, uamuzi wa Baraza ubatilishwe, na mgogoro usikilizwe upya kwa haki.
Wakili wa mjibu rufaa, alidai kuwa hukumu ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya akisema kuwa hakukuwa na kosa lolote la kisheria.
Amesema chini ya kifungu cha 13 (4) cha Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya haliruhusiwi kusikiliza na kuamua mgogoro wa ardhi isipokuwa Baraza la Kata limethibitisha kwamba limeshindwa kutatua suala hilo, na kuomba rufaa itupiliwe mbali na uamuzi wa awali ubaki kama ulivyo.
