Mfumo wa IDRAS kuunganishwa na AI, kulinda taarifa binafsi

Shinyanga. Katika kuboresha mfumo wa ukusanyaji kodi kwa wafanyabiashara kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeunganisha mfumo wa IDRAS pamoja na akili unde ili kumsaidia mlipakodi kupata majibu ya maswali kwa urahisi bila kwenda ofisini pamoja na kulinda taarifa zake.

Akizungumza leo Januari 27, 2026 katika mafunzo ya matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) kwa wafanyabiashara na walipakodi, mwenyekiti wa mafunzo ambaye ni Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro ameeleza kuwa hii inaongeza uwazi na uelewa kwa mlipaji na kumfanya kulipa kodi kwa hiari.

“Mfumo wetu umeunganishwa na Akili unde (AI) ambapo itasaidia moja kwa moja mlipakodi kuuliza na kupata majibu ya maswali yanayohusiana na kulipa kodi, pia, hii inamfanya kuwa huru na salama katika kutunza taarifa za mlipakodi,” amesema Maro.

Kwa upande wake, mwezeshaji kutoka TRA, Omary Mataw ameeleza namna ya kujisajili katika mfumo huo akisema mzazi ana uwezo wa kupata namba ya mlipakodi (TIN Number) ya mtoto, ambayo itaenda kwa mtoto akifikisha miaka 18, na kukamilisha usajili wa maelekezo mengine, pia, kwa wenye TIN watatakiwa kuweka upya nywila.

Mfumo wa IDRAS unatarajiwa kuanza Februari 9, 2026 ikiwa ni hatua ya kuboresha ulipaji kodi kuendana na maendeleo ya kidijitali, ukiwa na lengo la kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na uelewa kwa walipakodi kulipa kwa hiari, ambapo huduma kupitia mfumo utakuwa unafanyika kielektroniki kwa saa 24.