Shinyanga. Mtu mmoja amepoteza maisha na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha lori na basi la abiria. Ajali hiyo imetokea leo Januari 27, 2026 saa 12:30 asubuhi katika eneo la mnada wa Tinde, wilayani Shinyanga.
Ajali hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Kisire lililokuwa likitokea Kahama kwenda Mwanza, na lori lililokuwa limebeba shehena ya mchele.
Aliyefariki dunia ni dereva wa lori hilo, Hitayezu Elias (35), raia wa Rwanda.
Katika picha ni roli kilikuwa limebeba mchele kutoka Rwanda lililopata ajali lenye namba za usajili RAE 849 N.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa basi la Kisire aliyeshindwa kuchukua tahadhari.
Amesema basi hilo, lilipofika katika eneo la mnada wa Tinde, liligonga toroli la wauza matikiti kabla ya kugongana uso kwa uso na lori hilo.
“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi la Kisire. Baada ya ajali, dereva huyo alitoroka na Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtafuta ili achukuliwe hatua za kisheria,” amesema Kamanda Magomi.
Katika picha ni roli kilikuwa limebeba mchele kutoka Rwanda lililopata ajali lenye namba za usajili RAE 849 N.
Ameeleza kuwa basi hilo lilikuwa na jumla ya abiria 42, ambapo 12 walijeruhiwa. Kati yao, watano hali zao ni mbaya na wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwawaza, huku wengine saba wakipatiwa matibabu katika Zahanati ya Tinde.
Mmoja wa majeruhi, Robert Daudi, amesema alikuwa akisafiri na watoto wake watatu na waligundua kuwa wamepata ajali baada ya kusikia kishindo kikubwa.
Katika picha ni roli kilikuwa limebeba mchele kutoka Rwanda lililopata ajali lenye namba za usajili RAE 849 N.
“Nilikuwa nasafiri na watoto wangu watatu, ghafla nikasikia kishindo kikubwa ndipo tukagundua tumepata ajali. Nashukuru Mungu watoto wangu wako salama,” amesema Daudi.