Dar es Salaam. Shahidi wa tisa wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi mwanzilishi wa Kampuni ya Vanila International Limited, Simon Mkondya, maarufu kama Dk Manguruwe, na mwenzake John Rwezaula, ameieleza mahakama jinsi alivyoshawishika kuwekeza Sh20 milioni katika kampuni hiyo.
Shahidi huyo, Abeid Shekimweri, ametoa ushahidi wake leo Jumanne, Januari 27, 2026, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashitaka 28, yakiwemo ya kujipatia zaidi ya Sh90 milioni kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa viwanja tisa eneo la Idunda, mkoani Njombe.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Neema Kibodya, shahidi ameeleza kuwa aliwekeza Sh20 milioni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya vanila na yangiyangi, baada ya kushawishika na matangazo aliyoyaona katika vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, aliahidiwa kupata zaidi ya Sh120 milioni ndani ya mwaka mmoja na nusu.
Shahidi ameongeza kuwa baada ya matangazo hayo, aliwatafuta viongozi wa kampuni ya Vanila ambao walimwambia kuwa mashamba yao yapo Bungi, Zanzibar.
Alipofika ofisini, alipewa kabrasha lililoeleza aina ya mazao yanayolimwa na kampuni, kisha akaamua kuwekeza Sh12 milioni katika zao la vanila na Sh8 milioni katika zao la yangiyangi.
Kwa zao la vanila aliahidiwa faida ya Sh120 milioni baada ya mwaka mmoja na nusu, huku kwa zao la yangiyangi aliahidiwa kupata faida ya kila wiki mara baada ya kuvunwa kwa maua yake.
Hata hivyo, baada ya muda uliokubaliana kuisha, shahidi amesema alikwenda kutembelea mashamba, lakini hakukuta mazao wala shamba lolote.
Alipowatafuta wahusika, alielezwa atulie na kuwa kila kitu kitakuwa sawa.
“Baada ya kutulia vya kutosha, siku moja niliona katika vyombo vya habari kuwa Bwana Mkondya ameshtakiwa. Hivyo nilikwenda kituo cha polisi kutoa taarifa na kisha kuambiwa niende mahakamani,” amesema Shekimweri.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari 1, 2020, na Desemba 1, 2023, ndani ya Dar es Salaam.
Dk Manguruwe na mwenzake wanadaiwa kuendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi wawekezaji faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizowekeza, na kujipatia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19.
Aidha, Dk Manguruwe peke yake anadaiwa kununua viwanja tisa, kitalu namba AB, eneo la Idunda mkoani Njombe, akijua kuwa mali hizo ni zao la makosa ya awali ya upatu.