Unguja. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezitaka mamlaka za upimaji ardhi na upangaji miji nchini, kuhakikisha katika upimaji wa maeneo mapya wanatenga nafasi ya upandaji miti katika mipango ya makazi na matumizi ya ardhi.
Pia, amezitaka taasisi mbalimbali za umma na binafsi, kuhakikisha zinapanda angalau mti mmoja na kuhakikisha unatunzwa hadi kukua katika maeneo yao, ili kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumanne Januari 27, 2026 katika hotuba yake baada ya kupanda mti wakati akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa Januari 27, 1960. Amefikisha miaka 66. Pia, amekata keki ya kuadhimisha siku hii.
“Nizitake mamlaka za upimaji ardhi na upangaji miji nchini kote kuhakikisha katika upimaji wa maeneo mapya wanazingatia kutenga maeneo ya kijani na nafasi ya upandaji miti katika mipango ya makazi na matumizi ya ardhi,” amesema.
Katika hotuba yake hiyo, amesema mabadiliko ya tabianchi si hadithi wala maneno ya nadharia kwa sasa, bali ni uhalisia unaoonekana na tunaishi nao.
Ameeleza nchi nyingi duniani zinakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuongezeka kwa ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko, kuongezeka kwa joto na kina cha Bahari.
Kwa Tanzania, mkuu huyo wa nchi, amesema athari hizo zinagusa maisha ya moja kwa moja ya wananchi na ustawi wa Taifa ikiwemo kadhia ya kukosekana maji safi na salama na kuathiri uzalishaji wa chakula.
Upandaji miti, amesema ni moja ya njia zinazosaidia kukabili athari hizo, akisisitiza mti unaopandwa sasa utaleta mvua kwa vizazi vijavyo.
Amewataka wakuu wa mikoa na wilaya zenye maeneo yaliyoathirika, kusimamia upandaji miti na wasisubiri siku za matukio kufanya hivyo, ili kurudisha mazingira.
Amesema amechagua kupanda miti katika siku yake ya kuzaliwa ili kutimiza wajibu wake wa kuitunza na kuihifadhi dunia.
“Vilevile kuacha urithi kwa vizazi vinavyokuja. Sisi tulirithi uoto wa asili mwingi, tulirithi nchi yetu ikiwa haijaharibiwa kiasi hiki, tulirithi miti mingi ya matunda, iliyopandwa mashambani na ile inayojiotea,” amesema.
Hata hivyo, amesema kupanda miti, pamoja, unatekeleza malengo kadhaa ya Ajenda za Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), liliwemo lengo namba 13 linalotaka kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Pia, amesema kupanda miti kunatekeleza lengo namba 15 la SDG linaloeleza umuhimu wa kuuliza uhai katika ardhi na lengo namba mbili la kuondoa uhaba wa chakula.
Kupanda miti pia, amesema kunatekeleza lengo namba tatu la kustawisha afya na ustawi wa jamii na lengo namba sita la kuhifadhi maji.
Samia amesema kwa ujumla kutekelezwa kwa malengo yote hayo, kunatimiza lengo namba moja la kuondoa umaskini.
Ameeleza Tanzania ni sehemu ya juhudi za dunia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia mikataba mbalimbali ukiwemo wa Paris unaozitaka nchi wanachama kuchukua hatua za pamoja za kupunguza hewa ukaa.
Amesema wilaya zenye misitu mingi zimeanza kunufaika na biashara hiyo ikiwemo Tanganyika inayojenga shule zake na kufanya miradi mingine ya maendeleo.
Rais Samia amesema idadi ya Watanzania inakuwa na watafikia milioni 70 ikiwa, hivyo iwapo milioni 30 watapanda kila mtu mti mmoja kila mwaka, “tutakuwa na idadi kubwa ya miti kila mwaka na miaka michache Taifa litabadilika kwenda kwenye maliasili himilivu na uhimilivu wa mazingira.
Amesema ni wajibu na uzalendo kila mmoja atashiriki kufanikisha ajenda hii ya mazingira.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia utunzaji wa mazingira kukabiliana mabadiliko ya tabianchi kwani suala la mazingira ni miongoni mwa nguzo muhimu maendeleo ya uhifadhi, huku akiipongeza wizara ya Muungano na Mazingira kwamba imeanza kutekeleza dira ya maendeleo 2050.
Amesema msingi huo unahakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za asili na kuhakikisha uwezo wa Taifa wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Awali, katika mahojiano mafupi katika kipindi cha Jambo Tanzania TBC, Rais Samia amesema hali ya mazingira kuna mabadiliko makubwa kwani kile kilio cha hali ya jangwa hususani mikoa ya Shinyanga, Dodoma na ukanda wa kati lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa.
“Lakini upandaji wa miti sote ni mashahidi kwamba Dodoma inakwenda kuwa ya kijani kupitia kampeni tunayosema kuwa kila mtu akijenga apande miti miwili,” amesema.
Amesema kampeni ya upandaji wa miti kwa ujumla kama tunavyofanya ile Dodoma ya vumbi sasa haipo, kwa hiyo kwa kiasi fulani kuna mabadiliko.”
Hata hivyo, amesema wanapata changamoto ya mvua lakini jinsi inavyopandwa miti mingi hiyo hali inakwenda kubadilika.
Rais amewataka kujenga utamuduni wa kuhifadhi na kulinda mazingira na zaidi kurithisha utamaduni kwa watoto.
“Mtoto akipanda na akasimamia mti akiwa mdogo anakuwa na uchungu na mazingira kisha analinda maliasili za nchi yetu.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni amesema wanaendelea kutekeleza maagizo mbalimbali kuhakikisha kijani
Masauni amesema hivi karibuni wanatarajia kuzindua mkakati kabambe wa utunzaji mazingira nchini ambapo miti milioni 10 inatarajiwa kupandwa kupitia mkakati huo.
Pia wanatarajia kuanzisha na kufufua bustani za kijani ambapo zitakuwa katika hekta 200,000 nchi nzima.
“Hili linaonesha kwa namna gani tunaendelea kusimamia maagizo yako kuhakikisha kuna mabadiliko ya kijani hapa nchini kama unavyotaka,” amesema.
Pia amesema kwa kushirikiana na wizara ya nishati wanaendelea kusimamia biashara ya hewa ukaa ambapo wanatarajia kupata Dola za Marekani bilioni mbili kupitia biashara ya hewa ukaa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja (RC), Amida Mussa Khamis, amesema tangu waanze mpango huo wameshapanda miti 62,630 ya matunda na misitu.
Pia wamepanda miti 10,000 ya mikoko katika fukwe za bahari katika kuhifadhi.
Amesema katika eneo hilo la Bungi lilikuwa na changamoto na kwa siku ya leo wamepanda miti 1,705 kati ya hiyo 105 ni matunda na 1,600 ni misitu.
Naye Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema kitendo cha Rais Samia kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti, linapaswa kuigwa na wananchi kufanya mambo ya msingi katika kuadhimisha siku zao za kuzaliwa.
“Hili limetupa somo na elimu kwamba tutumie siku zetu za kumbukizi za kuzaliwa kusaidia jamii italeta faida kwa miaka mingi ijayo,” amesema Hamza.