Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewaagiza maofisa ardhi kuhakikisha kila anayepata hati ya kiwanja anapanda miti isiyopungua mitano, hatua inayolenga kurejesha uoto wa asili uliopotea kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kuunga mkono dhamira ya Serikali katika utunzaji wa mazingira.
Agizo hilo limetolewa leo, Januari 27, 2026, wakati wa sherehe za upandaji miti zilizofanyika katika Shule ya Sekondari Moshi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Babu aliambatana na Kamati ya Usalama ya mkoa ambapo pamoja na upandaji miti, pia walikata keki kusherehekea siku hiyo maalumu.
“Waheshimiwa wakuu wa wilaya, maofisa ardhi wanapaswa kuhakikisha kabla ya kutoa hati za viwanja, kila anayepata hati ya kiwanja anapanda miti isiyopungua mitano mbele ya nyumba yake au kuzunguka eneo lake,” amesema Babu, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kurejesha Kilimanjaro kuwa ya kijani na kuimarisha hali ya hewa.
Amesema kuwa kupanda miti kunaleta faida nyingi ikiwemo mvua za kutosha, hewa safi, harufu nzuri na utulivu wa mazingira.
“Kwa Mkoa wetu kwa sasa tunahitaji kila mmoja kushiriki kupanda miti. Haiwezekani mtu asipande mti mmoja na kusubiri wenzake wapande, tunahitaji Kilimanjaro ya kijani,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akiwa pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Moshi wakiwa wamenyanyua keki juu ikiwa ni sehemu ya kusherekea kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Picha na Janeth Joseph
Babu pia ameongeza kuwa Serikali inasisitiza utunzaji wa mazingira, ikiwa ni pamoja na upandaji miti, utunzaji wa misitu na vyanzo vya maji.
Mwaka 2025 Mkoa wa Kilimanjaro ulipanda miti 8,917 katika maeneo mbalimbali, hatua iliyotekeleza maagizo ya Rais Samia.
“Ni uzalendo kuhakikisha Kilimanjaro inarudi kuwa ya kijani. Kila mmoja anapaswa kushiriki,” amesema Babu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema jitihada za kupanda miti zinaendelea na kwamba miti inayopandwa itatunzwa ipasavyo kufanya Tanzania kuwa ya kijani.